Kocha wa Kaizer Chiefs, Nasredine Nabi amewatuliza mashabiki na mabosi wa Azam kwa kuwaambia wampe muda kocha mpya kwani ana kitu atawafikisha mbali.
Nabi ameyasema hayo baada ya kocha mpya wa Azam, Rachid Taoussi kuanza na suluhu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Taoussi ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja kuinoa Azam, amekuja kuchukua mikoba ya Youssoupha Dabo ambaye ameondolewa kutokana na matokeo mabaya iliyoyapata timu hiyo mwanzoni mwa msimu.
Akizungumzia ubora wa kocha Taoussi raia wa Morocco, Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa ni mwalimu bora ambaye Azam imempata akiamini kwamba ataibadilisha timu hiyo kwa kuipa mafanikio makubwa.
Nabi raia wa Tunisia ambaye aliwahi kuifundisha Yanga na FAR Rabat ya Morocco, alisema anamfahamu Taoussi ni kocha anayetamani mafanikio wakati wote huku akiwa si mtu anayefurahia kushindwa kupata ushindi muda mwingi akitumia falsafa za soka la kushambulia.
“Rachid namfahamu vizuri, ni kocha mkubwa ambaye Azam wamempata, huyu ni kocha anayetamani kushinda wakati wote, mtaona hata soka lake ni la kushambulia zaidi na nidhamu ya ulinzi,” alisema Nabi.
“Azam wanatakiwa kumpa muda aweze kuwabadilisha wachezaji kuwa bora na timu ishinde, wasipate wasiwasi na hiyo sare ya mechi ya kwanza, naamini Rachid atawapa ubora wa kupigania makombe.”
Katika hatua nyingine, Nabi alisema ili hayo yaende vizuri, wachezaji wa Azam wanapswa kujituma na kuwa na nidhamu kwani wanafundishwa na kocha mwenye misimamo mikali. “Wachezaji wa Azam wanatakiwa wajiandae kwa kujituma. Huyu sio kocha anayetaka wachezaji wasiojituma, ana misimamo mikali katika kusimamia nidhamu kwenye timu yake.”