Msaani wa Muziki wa Kizazi Kipya (Bongo Flava) Emmanuel Elibariki maarufu kama Nay wa Mitego, ameitikia wito wa kufika kwenye ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Nay aliitikia wito huo mara baada ya kupokea barua, kuhusiana na wimbo wake wa nitasema na kukutwa na makosa manne.
Kosa la kwanza ni kukiuka maadili, kosa la pili ni uchochezi dhidi ya serikali, kosa la tatu ni kuaminisha jamii rais hafanyi kazi na kosa la nne ni kuikashifu Rwanda na Congo.
"BASATA wamenipa notisi nitaweka kila kitu mtandaoni. Mimi ni sauti ya wengi na sauti ya Mungu. Sina cha kuwalipa mashabiki zaidi ya kufanya hiki ninachokifanya kwa maana ya kuwasemea. Sitonyamaza, hili ni la kwao, waendelee kunisapoti na inaonesha kila ninachokifanya inaonesha ndicho wanakitaka," amesema Nay.
Aidha, Wakili wa Nay, Jebra Kambole amesema BASATA wamemshitaki msanii huyo kwa makosa manne ikiwemo kutoa wimbo bila kuwa na kibali cha BASATA, ametoa maneno ambayo ni ya uchochezi katika wimbo wake 'Unasema' serikali inahusika na utekaji na mauaji.
"Kosa la tatu ni kutoa maneno ya upotoshaji kuwa kuna miradi iliyoanzishwa na haiendelei na kosa la nne wamesema ametoa maneno kuwa amekashifu mataifa mengine na kwamba yanaweza kuleta mgogoro.
"Kutokana na makosa haya tunatakiwa kuleta maelezo ya kina kuhusu mashitaka hayo. BASATA ndiyo wamemshitaki, ndio watakaoendesha mashitaka na ndiyo wanao watakaotoa hukumu, mnaweza kuona sheria za nchi yetu," amesema Kambore