Mwanamuziki wa muziki wa hip-hop Sean "Diddy" Combs amenyimwa dhamana tena baada ya mawakili wake kubishana kwa mara ya pili kwamba anapaswa kuachiliwa kutoka kwenye hali "ya kutisha" ya jela wakati akisubiri kesi ya biashara ya ngono inayomkabili.
Jaji wa shirikisho mjini New York alimuweka rumande mwanamuziki huyo siku ya Jumanne baada ya waendesha mashtaka kudai kwamba kulikuwa na "hatari kubwa ya [mshukiwa] kutoroka".
Bw Combs, 54, alikamatwa wiki hii, akishutumiwa kwa kuendesha biashara ya uhalifu kuanzia mwaka 2008 iliyohusisha dawa za kulevya na unyanyasaji ili kuwalazimisha wanawake "kutimiza tamaa zake za ngono", kulingana na waendesha mashtaka.
Combs amekana mashtaka yote.
Baada ya uamuzi huo, wakili wa Bw Combs, Marc Agnifilo, aliwaambia waandishi wa habari kwamba uamuzi huo "haukuenda tunavyotaka," na kuongeza "mapambano yanaendelea".
Shtaka la kurasa 14 linamshtaki Bw Combs kwa ulaghai, biashara ya ngono kwa nguvu na usafiririshaji haramu wa watu ili kwa ajili ya kutumikishwa ukahaba.
Iwapo atapatikana na hatia ya makosa yote matatu, rapa huyo na mtayarishaji rekodi anakabiliwa na kifungo cha miaka 15 hadi kifungo cha maisha jela.