Namna maisha yanavyokwenda kasi. Mbwana Ally Samatta aliuzwa kwenda TP Mazembe kwa Dola 100,000 miaka 13 iliyopita. Ilikuwa pesa nyingi wakati huo. Moise Katumbi aliamua kuondoka na mtu wake baada kumsumbua katika mechi mbili zilizochezwa Lubumbashi kisha pale Dar es Salaam.
Naambiwa tu mashabiki wa Mazembe ambao walisafiri kwa wingi mpaka Dar es salaam ndiyo ambao walilazimisha tajiri wao amchukue Samatta ambaye alikuwa ametakata vilivyo. Kwa wakati huo ilikuwa pesa nyingi. Simba walikuwa chini ya kundi la Friends of Simba.
Miaka kadhaa baadaye kuna mshambuliaji mwingine wa Tanzania, Clement Mzize naye anatakiwa. Yanga wamegomea hadi dau la Dola 300,000 kutoka kwa Waydad Casablanca ya Morocco. Kocha Rhulani Mokwena anakosa usingizi kwa sababu ya Mzize. Siyo yeye tu, klabu mbalimbali zinaonekana kumtaka mshambuliaji huyo anayeng'ara kwa sasa.
Namna maisha yalivyobadilika. Naambiwa Yanga wanataka Dola 1 milioni kumuuza Mzize. Kiburi hiki kinatoka wapi? Mzize anastahili kuuzwa hivyo? Inawezekana. Kilicholeta kiburi hicho ni kwamba tayari timu zetu zimeanza kufanya manunuzi ya wachezaji wa bei ghali. Ama kwa kuwalipa 'signing fee' au kwa kuwanunua kutoka katika klabu zao.
Awali Waydad walitaka kulipa Dola 100,000 kwa Mzize. Naamini ulikuwa utoto kutoka kwao. Dola 100,000 inawezekana ni kiasi ambacho Yanga wametumia kuongeza mkataba wa Djigui Diarra. Siyo Yanga tu, sioni kama Simba wangemuuza Samatta wa leo kwa dau la Dola 100,000. Matumizi ya klabu yamekwenda juu kiasi kwamba hauwezi kuwachezea tena kwa kiasi cha Dola 100,000.
Kuanzia mwaka ule ambao Samatta aliuzwa hadi leo, klabu zetu zimeanza kupata fedha nyingi kutoka katika vyanzo mbalimbali kiasi kwamba Dola 100,000 imeanza kuonekana kuwa pesa kidogo. Klabu zina mabilioni ya wadhamini wanaokaa kifuani, haki za matangazo, viingilio na wadhamini wengine mbalimbali. Dola 100,000 imeanza kuwa kidogo.
Wakati ule Simba wakimuuza Samatta tegemeo kubwa kipesa lilikuwa ni kwa watu wa Friends of Simba na vyanzo vichache vya pesa. Dola 100,000 ilikuwa pesa nyingi ya kuisukuma klabu mbele. Kwa sasa ni pesa ndogo ambayo hata wao wenyewe wameweza kumnunua mchezaji kama Joshua Mutale.
Hapohapo naamini kuna tatizo kubwa la washambuliaji barani Afrika na duniani kwa ujumla. Yanga wanaweza kumuuza Mzize hata kwa Dola 1 milioni kama akiendelea kuimarika. Washambuliaji wenyewe wako wapi? Msimu uliopita wakati Fiston Mayele akitesa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika nilifahamu kwamba lazima angetakiwa na wakubwa. Kuna uhaba wa washambuliaji.
Kwa hiki anachoendelea kukionyesha Mzize ni suala la muda tu kabla hajauzwa pesa nyingi. Unapata wapi mshambuliaji mwenye nguvu, kasi, stamina, umbo kubwa na anayejua kuziona nyavu? Akitokea mchezaji wa namna hiyo kwa sasa moja kwa moja anakwenda sokoni kirahisi. Ni suala la muda tu kabla hajaondoka zake.
Lakini hapo hapo kuna jambo jingine ambalo hauwezi kuliona kwa macho. Kuanzia wakati ule Samatta anauzwa hadi leo Mzize anatakiwa nadhani klabu zetu zimebadili madhumuni yake katika michuano ya kimataifa. Klabu zetu zinaamini zinaweza kwenda fainali ya michuano ya CAF na ikiwezekana kutwaa ubingwa. Wanahisi kwa kumuuza mchezaji kama Mzize unaondoa makali ya kufikia lengo.
Simba hawakutafakari hivyo wakati walipomuuza Samatta. Kwa wakati huo hata kufika robo fainali ilikuwa ngumu. Hawakuwa na ndoto sana ya kufika mbali katika michuano ya kimataifa kwa sababu kina Al Ahly walikuwa wameshika hatamu hasa. Baadaye wakati ndoto zimeanza kuja kichwani walilazimika kuwauza Jose Luis Miquissone na Clatous Chotta Chama kwa bei ya lazima.
Yanga wanatumia kiburi cha kubakisha wachezaji walio bora kama Mzize kwa sababu wameanza kuota ndoto ya taji la ubingwa. Hata hivyo kuna wakati watalazimika kumuuza kama wakubwa wakiendelea kutanua mbavu. Wakati mwingine kikwazo kikubwa kwa wachezaji wetu inakuwa ni mishahara. Unaweza ukapambana na dau la kumuuza lakini bado hatuna mbavu za kupambana na dau la mshahara.
Manufaa kwa taifa? Kama Mzize akienda nje akacheza katika klabu imara zaidi ya Yanga kama TP Mazembe ilivyokuwa imara zaidi kwa wakati ule kuliko Simba, basi kutakuwa na manufaa makubwa kwa taifa. Nadhani anaweza kuwa mshambuliaji namba moja wa Taifa Stars kama tukifuzu kwenda Afcon mwakani pale Morocco.
Lakini miaka miwili baadaye anaweza kuwa mshambuliaji namba moja wa Stars wakati Tanzania itakapokuwa mwenyeji wa Afcon sambamba na Uganda na Kenya. Kama akiendelea na moto huu huu atakuwa chaguo la kwanza kwa Stars kwa miaka mingi ijayo wakati huu kina Samatta na Simon Msuva wakielekea ukingoni.
Kwa Mzize mwenyewe? Amepiga hatua kubwa. Amepiga hatua kubwa katika maisha yake binafsi. Ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengi kote nchini. Kutoka kuendesha bodaboda mpaka kuwa mmoja kati ya washambuliaji hatari Afrika. Muda siyo mrefu ataendesha Range Rover yake binafsi. Ni namna ambavyo maisha yanakwenda kasi.
Kwa sasa aimarike zaidi katika kutupia mpira wavuni. Msimu huu anaonekana kuwa na jicho la lango kitu ambacho kilikuwa udhaifu kwake hapo awali. Sifa nyingine zote za mshambuliaji hatari anazo kama nilivyobainisha hapo juu. Ana kasi, nguvu, stamina. Mwili wake pia ni tishio kwa mabeki wengi ambao wanapambana naye.
Zaidi ya kila kitu asivimbe kichwa. Ametoka mbali. Kupenya katika kikosi kikali cha Yanga ukitokea timu ya vijana siyo jambo la kawaida kwa timu zetu ambazo kwa sasa akili zimewekeza zaidi katika kuleta mastaa wa kigeni kutoka nchi zilizoendelea kisoka.