RAIS SAMIA ACHARUKA WANAOMWITA MUUAJI

 

RAIS SAMIA ACHARUKA WANAOMWITA MUUAJI

Rais Samia Suluhu Hassan ameupa rungu Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa CCM, kuwajibu wanaozungumza vibaya dhidi yake, akisisitiza hawapaswi kuhofia.


Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, ameikabidhi UWT jukumu hilo akisema wakati mwingine mdomo wake pekee na wingi wa majukumu aliyonayo hapati muda wa kuwajibu watu hao.


Ameeleza wanapoambiwa Mwenyekiti (Rais Samia) ni muuaji, wanapaswa kukiri kwa kusema ameua nguvu hasi ya upinzani.


Amesema hayo leo Jumamosi Septemba 28, 2024 alipofunga kikao maalumu cha UWT Taifa kilichofanyika wilayani Songea mkoani Ruvuma.


“Ombi langu kwenu (UWT) ni kusimama imara, ukweli mnaujua. Mdomo wa mwenyekiti mmoja kujibu hoja zile hautoshelezi na pengine mwenyekiti wakati mambo yale yanatoka nipo kwenye majukumu mengine, msimame tu mjibu mnahofia nini,” amesema.


Amesema wakiambiwa mwenyekiti wao ni muuaji wanapaswa kujibu ameua njia zote za kuzidisha umasikini katika nchi na amekuza uchumi.


Rais Samia amewataka kujibu ni kweli ameua giza lililokuwa limegubika Tanzania na sasa nchi ipo katika kiwango cha kimataifa cha kung’aa.


“Hayo ndiyo niliyoua Rais wenu na mwenyekiti wenu, sijawahi kuua mtu labda sisimizi nimeua, lakini siyo mtu. Kwa hiyo ndugu zangu simameni tu mjibu,” amesema.


Amesema maneno dhidi yake ni matokeo ya wazungumzaji kukosa pa kushika na kilichobaki wanaishia kutafuta lugha chafu za kumtupia.


Samia amesema mabadiliko na mageuzi yote yanayofanywa ndani ya CCM kwa ngazi zote yanalenga kukiimarisha.


“Niwahakikishie viongozi mabadiliko yote yanayotokea ni kukiimarisha chama tukitambua kwamba, bado hatujapata chama mbadala cha kuliongoza Taifa hili, bado hatujapata,” amesema.


Amesema mageuzi yamefanywa katika katiba, kanuni na hata vitendea kazi na kwamba, hatarajii kuona kwa kazi iliyofanywa inatokea CCM inashinda chini ya asilimia 80 katika chaguzi.


Safu imara


Amesema kwa kuwa nchi inaelekea katika chaguzi, jumuiya hiyo inapaswa kuhakikisha ushindi wa chama hicho kwa kuwa ni amri inayotolewa na katiba.


“Mmeimba hapa rafiki wa mwanamke ni mwanamke, chaguzi hizi na mmesema mmejipanga kwenda kwenye chaguzi. Niwaombe sana chaguzi hizi zisiende kupangua umoja wetu.


“Twende tukaangalie nani anafaa wapi, siyo kwenda kupelekanapelekana mambo ya uwifi na ushemeji, twende tukawapeleke wale wanaofaa,” amesema.


Amesema anatambua uhalisia na kwamba tayari watu wameshaanza kupanga vitenge na fedha kwa ajili ya kugawa kwa wapigakura. Amesisitiza kusaidiwa wasio na uwezo ili washinde.


“Nasisitiza safu itakayokivusha CCM na si safu itakayowavusha watu. Mkiweka safu za kuvusha watu mwisho wa uchaguzi hazitakuwa na kazi, ndiyo maana tulirudishwa nyuma sana huko nyuma,” amesema.


Pia ameitaka UWT kuyaratibu makundi yote yanayoisemea vema Serikali lakini nje ya jumuiya hiyo ili ishirikiane nayo kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.


“Kuna makundi mengi sijui kuna watu wanaitwa wanawake 100,000 kuna wanawake na Samia sijui marafiki wa Samia mambo mengi, wengine vijana wa kike wapo kwenye kundi linaitwa TK Movement ni vijana wazuri wanalisemea Taifa wavuteni, muwe nao badala ya kubishana nao,” amesema.


Awali, Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda aliwashangaa wanaodai hakuna kilichofanywa na Serikali.


Chatanda amesema wanaotoa kauli hizo watafsiriwe kuwa hawalijui walitendalo, kwa kuwa kazi zilizofanywa na Serikali zinaonekana katika maeneo mbalimbali.


Ameeleza kuchukizwa na hatua ya wanawake wa Chadema ya kumwita Rais Samia ni muuaji, akiwataka waombe radhi.


Hata hivyo, amesema jumuiya hiyo haiungi mkono vitendo vya utekaji na mauaji, akitaka vyombo vya usalama kufuatilia kwa karibu.


Amesema licha ya juhudi zinazofanywa na kustawisha siasa nchini, kuna chama alichosema kinajipa umuhimu.


“Kuna chama kinataka kusikilizwa matakwa yao tu, kinataka kuonekana bora kuliko vingine, kinajipa umuhimu kuliko vingine. Sasa wametikisa kiberiti wamekuta kimejaa na kina njiti na njiti zake zinawaka,” amesema.


Kuelekeza uchaguzi wa serikali za mitaa, Chatanda ameomba CCM kutoa maelekezo kwa ngazi za chini kuwateua wanawake wenye uwezo wa kugombea kwa angalau asilimia 30 ili waongezeke katika ngazi za maamuzi.


Chatanda amesema katika kipindi cha miaka miwili kutoka mwaka 2022 hadi Septemba mwaka 2024, jumuiya hiyo imesajili wanachama wapya 4,117,030.


Idadi hiyo amesema imefanya jumla ya wanachama wa jumuiya hiyo ifikie 6,130,317, huku wanachama 3,484,892 wakisajiliwa katika mfumo mpya.


Amesema mpango wa jumuiya hiyo ni kuhakikisha kufikia Juni mwakani iwe imesajili wanachama milioni 12 ambao kimsingi watakuwa wapigakura.


Pia amesema UWT inalenga kujenga jengo la makumbusho ya Bibi Titi Mohamed na wanawake wengine waliowahi kuiongoza jumuiya hiyo.


Jengo hilo pia litatumika kuhifadhi kumbukumbu za historia ya Rais wa kwanza mwanamke nchini, Samia Suluhu Hassan na tayari walishaomba eneo kwa CCM jijini Dodoma kwa ajili ya utekelezaji.


Ndani ya jingo hilo amesema kutakuwa na mgahawa utakaotumika kama kitega uchumi na kuiingizia jumuiya hiyo mapato.


 Chanzo: Mwananch

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad