Mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, Mkuu ww Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda ametangaza kukabidhi majina ya watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakifanya ubadhirifu wa kutoa leseni mbalimbali za biashara kinyume na sheria.
Makonda ametoa kauli hiyo Septemba 19, 2024 wakati akimkaribisha Waziri Mchengerwa kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, ikiwa ni siku ya nne ya ziara ya Waziri huyo wa TAMISEMI ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Arusha.
Aidha Makonda amemtaja Mchengerwa kama kiongozi mwenye majibu ya changamoto mbalimbali za wananchi akionesha pia namna ambavyo wizara ya TAMISEMI imekuwa faraja na msuluhishi wa changamoto za wananchi wa maeneo mbalimbali.
Paul Christian Makonda amemshukuru pia Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na mfumo wa kidigitali wa manunuzi na ugavi wa Umma NeST na kusema mfumo huo umekuza uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha katika shughuli mbalimbali za kiserikali.