\
Simba waliwasili Tripoli miaka 13 tangu kuuawa kwa Rais wa zamani wa Libya, mwenye nchi yake. Muammar Muhammad Abu Minyar Al Gaddafi. Bado haikuwa sehemu salama kwa Simba ndani na nje ya uwanja.
Nje ya uwanja unaweza kujua kwanini Walibya waliwahi kufungiwa wasicheze na mashabiki. Wana shangwe ambalo limeambatana na vurugu. Walidhihirisha kwa wachezaji wa Simba. Walifanikiwa kufanya vurugu ikiwemo kuwarushia chupa wachezaji wa Simba.
Simba walionyesha kwamba wanafufuka. Kwanza kwa namna ambavyo walicheza kwa ari na kitimu. Kocha Fadlu Davids ameonyesha anatengeneza timu ambayo inashindindana.
Sina hofu sana kwamba miezi 15 iliyopita Simba wangeweza kupoteza pambano Tripoli. Namna ambavyo wenyewe walikuwa wanaonana ingewapoteza Simba mapema. Lakini, Simba hii mpya inacheza kitimu na mchezaji mmoja mmoja kuna ongezeko kubwa.
Kitimu ni namna ambavyo waliweza kuwazuia wenyeji wasipate bao kwa dakika tisini mbele ya mshambuliaji wao hatari, Agostinho Mabululu. Walijipanga wengi mbele ya mpira na kwa ushirikiano uliotukuka.
Na hapo Inaanzia kwa kipa wa Simba, Moussa Camara. Ametulia. Mtu wa kwanza ambaye hapaswi kutetemeka katika mazingira kama haya ni kipa. Anaweza kufungwa kwa kutetemeka tu.
Mara ya mwisho Simba kufanya vizuri katika mazingira ya chuki kipa alikuwa nyota wao wa mchezo, Juma Kaseja, mwaka 2003 wakati Simba walipowatoa Zamalek ugenini. Camara hakutetemeka.
Ameandika Mtaalamu wa uchambuzi, Legend Edo Kumwembe.