SIMBA YAMTAKA FEI TOTO CAF KWA UDI NA UVUMBA

 

SIMBA YAMTAKA FEI TOTO CAF KWA UDI NA UVUMBA

Wakati ikikamilisha mipango ya kumnasa winga, Elie Mpanzu, aliyemaliza mkataba na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Simba inatajwa sasa imehamishia nguvu zake kumnasa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' huku ikimhusisha kipa, Aishi Manula 'Tanzania One'.


Habari zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Simba inataka kubadilishana wachezaji, ikijipanga kumwachia Manula aende Azam ili impate Fei Toto pamoja na fedha.


Chanzo chetu kinadai Simba iko tayari kulipa kiasi cha Sh. milioni 350 katika kuhakikisha mchakato huo wa usajili unafanikiwa.


Taarifa zaidi zinasema Simba imeamua kutengeneza mtego huo kwa sababu ya mahitaji ya kila timu, ambapo wao wanamhitaji kwa udi na uvumba Fei Toto huku Azam FC ikitaka huduma ya Manula ili kufikia malengo.


Chanzo hicho kiliongeza tayari Simba imeanza mchakato wa usajili kutokana na kutinga hatua ya makundi katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo inaruhusiwa kufanya uhamisho, ingawa uhalali wake utaidhinishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), wakati wa dirisha dogo la usajili.


"Mwanzo Azam ilileta barua Simba kumhitaji Manula kwa mkopo, lakini Simba ilikataa ikataka imnunue moja kwa moja, kwa maana hiyo mpaka sasa bado wanamhitaji, na viongozi wetu pia wanamhitaji sana Fei Toto, kwa maana hiyo wamekaa na kuamua kufanya usajili wa kubadilishana wachezaji na pesa juu.


Nadhani hili sasa linaweza kufanikiwa, tusubiri mwezi Desemba na Januari mambo yanaweza kubadilika kabisa, Manula akaenda Azam na Fei Toto akatua Simba," alisema mtoa taarifa huyo.


Simba inataka kuwaongeza Mpanzu kwenye eneo la winga na Fei Toto sehemu ya kiungo mshambuliaji ili kukiongezea nguvu kikosi chake, hayo yamesemwa na Rais na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo'.


Mwekezaji huyo amesema anataka kuona Simba inafika fainali au inatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikiwa ni maandalizi ya kuwa na kikosi imara kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.


Mpanzu alikuwepo nchini hivi karibuni na alionekana katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita na Mnyama kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli kutoka Libya.


Fei Toto, katika mahojiano yake mara kwa mara amekuwa akisisitiza yeye ni mchezaji, anaweza kukipiga popote pale ambapo waajiri wake wa sasa Azam wataamua aende baada ya klabu hiyo kukamilisha uhamisho watakaokubaliana.


Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kwa sasa dirisha la usajili limefungwa, hivyo masuala hayo yatazungumzwa itakapofika kipindi hicho.


Ofisa huyo alisema kwa sasa akili na nguvu za viongozi wa klabu hiyo wamezielekeza katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoko mbele yao baada ya kumalizika kwa mechi za kimataifa za CAF.


"Kwa sasa tumemaliza michezo ya kimataifa, tuna Ligi Kuu, masuala ya usajili umepita tayari na tutauzungumza pale utakapokuja tena mwezi Desemba, tutaona nani kaingia, kama Mpanzu au mwingine yoyote," alisema Ahmed.


Baada ya mechi ya jana usiku, Simba itarejea Tanzania Bara na kuelekea Dodoma kuwafuata wenyeji Dodoma Jiji FC kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad