Simba, Yanga Kuweka Rekodi CAF

 

Simba, Yanga Kuweka Rekodi CAF

Wikiendi hii Yanga na Simba zina mechi za kuamua hatma zao katika michuano ya kimataifa kila mmoja akipambania rekodi zake.


Wakati wakipambania rekodi, kuna matumaini makubwa yapo kuanzia kwa wachezaji, viongozi, makocha hadi mashabiki, asilimia kubwa ya kutoboa ipo wazi.


Jeuri hiyo inakuja kufuatia rekodi nzuri walizonazo wawakilishi hao wa Tanzania waliosalia katika michuano ya kimataifa msimu huu.


Kesho Jumamosi, Yanga inacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE SA ya Ethiopia baada ya ugenini kushinda 1-0 na imeupeleka Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex ukitarajiwa kuchezwa saa 2:30 usiku.


Simba yenyewe itacheza Jumapili Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam sehemu ambayo wamekuwa wakijiona ni salama zaidi kwao linapokuja suala la mechi za kimataifa.


Hapa Simba itapambana na Al Ahli Tripoli ya Libya ukiwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ugenini matokeo kuwa 0-0.


SIMBA FRESHI


Katika misimu sita iliyopita, Wekundu hao walikuwa na rekodi ya kuvutia wakiwa nyumbani katika michezo ya maamuzi kabla ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Simba imekwama mara moja tu, ikiwa kwa Mkapa katika mechi za maamuzi ili kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa, jambo linaloonyesha uthabiti na uwezo wa kukabiliana na viunzi vya hatua hiyo. 


Msimu wa 2018-19 ulikuwa wa kihistoria kwa Simba. Baada ya kushindwa na Nkana kwa mabao 2-1 ikiwa ugenini Zambia, ilirejea kwa kishindo Kwa Mkapa na kuwachakaza wapinzani kwa mabao 3-1.


Ushindi huo haukuwa wa kawaida, kwani ulionyesha ujasiri wa Simba na uwezo wa kupindua matokeo.  Msimu huo, Simba iliendelea kucheza kwa kiwango cha juu hadi kufikia robo fainali, rekodi ambayo bado inasalia kuwa moja ya mafanikio makubwa kwa klabu hiyo katika michuano ya Afrika.


Hata hivyo, msimu wa 2019-20 ulikuja na changamoto zake. Simba, chini ya kocha Patrick Aussems, walijikuta wakitupwa nje ya michuano hiyo na UD Songo ya Msumbiji tena hatua za awali walishinda hata kufika katika mechi za maamuzi.


Baada ya sare tasa ugenini, Simba walishindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani walipotoka sare ya 1-1 na kutolewa kwa kanuni ya bao la ugenini. Ni pigo lililowafanya Simba kuelewa kuwa michuano ya Afrika inahitaji nidhamu na umakini wa hali ya juu.


Simba walifanya maboresho makubwa msimu uliofuata (2020-21). Usajili wa Luis Miquissone kutoka UD Songo ulikuwa na mchango mkubwa katika kuibeba timu hiyo, hasa katika mchujo dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe. Baada ya kupoteza 1-0 Zimbabwe, Simba walirejea kwa kishindo katika Uwanja wa Mkapa na kuwachapa wapinzani kwa mabao 4-0, ushindi uliowafikisha hatua ya makundi.


Msimu wa 2021-22 ulikuwa na machungu kwa mashabiki wa Simba. Baada ya ushindi mnono wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, wengi walidhani kuwa tiketi ya hatua ya makundi ilikuwa tayari mfukoni.  Hata hivyo, mchezo wa marudiano ulileta mshangao mkubwa baada ya Simba kuchapwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa na kutupwa nje ya michuano hiyo. Pigo hilo lilikuwa fundisho kwa Simbana walijitathmini na kurejea kwa nguvu katika michuano mingine, wakifika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.


Katika misimu miwili ya hivi karibuni (2022-23 na 2023-24), Simba wameonyesha ujasiri na nidhamu ya hali ya juu kwenye mechi za maamuzi. Ushindi dhidi ya C.D. Primeiro de Agosto ya Angola walishinda bao 1-0 nyumbani (ushindi wa jumla 4-1)  na Power Dynamos walitoa sare ya 1-1 nyumbani walipita kwa kanuni ya mabao ya ugenini, mechi ya kwanza walitoka 2-2


MSIKIE FADLU


Kocha wa Simba, Fadlu Davids anaamini wachezaji wanaweza kufanya vyema katika mchezo huo wa maamuzi dhidi ya Al Ahli Tripoli.


“Itakuwa mechi tofauti kabisa, tutatakiwa kuwa na nidhamu kubwa katika kulinda na kushambulia. Tuna faida ya kuwa nyumbani, hivyo nitoe wito kwa mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi. Itakuwa mechi nzuri na kuvutia, kwetu ni kama kazi itaanza upya.”


BWALYA AKAZIA


Mchezaji wa zamani wa Simba, Rally Bwalya, hakusita kutoa neno la faraja kwa klabu yake ya zamani. “Nakumbuka jinsi mashabiki walivyokuwa wakitufanya kujituma zaidi kutokana na sapoti yao. Simba ina nafasi ya kwenda makundi,” alisema Bwalya.


Katika mchezo huo wa maamuzi dhidi ya Al Ahli Tripoli, Simba wanajua wazi ushindi utawahakikishia tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo kocha Fadlu na vijana wake watalazimika kuonyesha nidhamu, umoja na uwezo mzuri wa kiufundi ili kupata matokeo mazuri.


YANGA NAKO


Wakati Simba wakifanikiwa kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara tano katika misimu sita iliyopita, wenzao Yanga ndani ya muda huo wametinga makundi mara mbili pekee.


Yanga katika mara mbili walizowahi kucheza makundi, zote wamekuvuka hapo na angalau kucheza robo fainali kama ilivyotokea msimu uliopita Ligi ya Mabingwa Afrika.


Mafanikio yao makubwa zaidi katika kipindi hicho ni msimu wa 2022-2023, walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuteleza Ligi ya Mabingwa na mechi za mtoano walipigwa na Al Hilal ya Sudan jumla ya mabao 2-1. Walivyoangukia Shirikisho hawakushikika hadi fainali.


Katika msimu wa 2018-19, Yanga haikushiriki kimataifa lakini 2019-20 ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika ikaishia hatua ya pili baada ya kuondolewa na Zesco ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2. Mechi ya kwanza nyumbani matokeo 1-1, ugenini Zesco ikashinda 2-1.


Kabla ya hapo, hatua ya awali Yanga iliwatoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1. Nyumbani ilikuwa 1-1, ugenini Yanga ikashinda 1-0.


Msimu wa 2021-22, Yanga iliishia hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-0 na Rivers United ya Nigeria baada ya kichapo cha bao 1-0 nyumbani na ugenini.


Katika msimu ambao ulikuwa wa kihistoria zaidi kwa Yanga ni 2022-23 na licha ya kutofanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa, walipoangukia Shirikisho walifika hadi fainali.


Yanga msimu huo ilianzia Ligi ya Mabingwa kwa kuifunga Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, kisha hatua ya kwanza ikafungwa na Al Ahilal ya Sudan jumla ya mabao 2-1. Nyumbani Yanga ililazimishwa sare ya 1-1, ilipoenda ugenini ikafungwa 1-0.


Kwa bahati, zamani mfumo uliowekwa na CAF ni kwamba timu zikiondolewa hatua ya pili katika Ligi ya Mabingwa, zinakwenda kucheza mtoano Shirikisho kupambania nafasi ya kuingia makundi katika michuano hiyo ya pili ngazi ya klabu barani Afrika.


Mtoano Yanga ilipangwa dhidi ya Waarabu Club Africain kutoka Tunisia, hapa nyumbani matokeo yalikuwa 0-0, ugenini ndipo Yanga wakaenda kufanya maajabu kwa kushinda bao 1-0 lililofungwa na Stephane Aziz Ki dakika ya 79. Wakafuzu makundi ambapo walikwenda kucheza hadi fainali ya michuano hiyo.


Yanga walikaribia kulibeba kombe hilo, lakini sheria ya bao la ugenini ikawahukumu kwani matokeo ya jumla yalikuwa 2-2 dhidi ya USM Alger ya Algeria. Nyumbani walifungwa 2-1, ugenini wakashinda 1-0.


Msimu uliopita 2023-24, wakarejea tena Ligi ya Mabingwa wakianzia hatua ya awali wakiiondosha Djibouti Telecom kwa jumla ya mabao 7-1. Hatua ya pili wakaichapa Al Merrikh ya Sudan jumla ya mabao 3-0.


Ugenini walishinda 2-0 na nyumbani 1-0. Wakafuzu makundi na safari yao ikaishia robo fainali walipoondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa penalti 3-1 baada ya kushindwa kufungana mechi zote mbili nyumbani na ugenini.


Ukiachana na rekodi hizo, kitendo cha Yanga kucheza nyumbani mechi ya maamuzi dhidi ya timu kutoka Ethiopia nacho kinawapa matumaini makubwa. Rekodi zinaonyesha kwamba, Yanga imecheza mara nne nyumbani dhidi ya Wahabeshi na haijapoteza hata moja. Imeshinda tatu na sare moja.


Katika mechi hizo, imezifunga St. George (5-0), Coffee (6-1), Welaita Dicha (2-0) na sare ya 4-4 dhidi ya Dedebit.


Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya CBE, amesema wamefanyia marekebisho makosa yaliyotokea ugenini waliposhinda bao 1-0 huku wakikosa nafasi zaidi ya saba za wazi kufunga mabao.


“Sote hatukufurahia kile kilichotokea Ethiopia, ilitakiwa kushinda kwa kiwango kikubwa lakini mambo haya yanatokea kwenye soka, ninachofurahia kila mchezaji anajutia lile.


“Tumefanya mazoezi ya kutosha ya kufunga mabao, naweza kusema kila kilichofanywa na washambuliaji na wachezaji wa nafasi nyingine kimenivutia sana naamini tutakwenda kuwa na dakika 90 nzuri nyumbani mbele ya mashabiki wetu,” alisema Gamondi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad