Simu zinaita.. Kocha Juma Mgunda Alivyoweka Heshima Simba

 

Simu zinaita.. Kocha Juma Mgunda Alivyoweka Heshima Simba

Kwa sasa simu zinaita tu kwa kocha, Juma Mgunda, ambaye alihudumu katika klabu ya Simba kwa miaka miwili sawa na siku 732, kuanzia Septemba 7, 2022 aliporithi kwa muda mikoba ya Zoran Maki ambaye alitimkia Al Ittihad ya Misri na kuweka rekodi za kibabe.


Uteuzi wa Mgunda kutoka Coastal Union awali ulitajwa ni wa kuokoa jahazi kwa kuisimamia timu kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.


Kazi aliyoifanya kwenye mchezo huo na mingine iliyofuata katika ligi iliwafunga midomo waliouponda uteuzi wake, kwani namba zilimbeba na kuwafunika baadhi ya makocha wa kigeni walioinoa timu hiyo.


MWANZO WAKE

Tangu Mgunda aanze kazi Msimbazi dhidi ya Nyasa Big Bullet ugenini katika mchezo wa kimataifa na kushinda 2-0, alithibitisha ni mtu wa kazi kwani mechi iliyofuata alivunja mwiko dhidi ya Tanzania Prisons kwa kuwachapa bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara.


Iliporudiana na Big Bullets jijini Dar, Simba ikashinda tena 2-0 na kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya ngazi ya klabu Afrika na baadaye ikacheza Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda mabao 3-0.


Baada ya hapo ikaenda kambini visiwani Zanzibar na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Malindi na Kipanga na kuzifunga mabao 1-0 na 3-0 mtawalia kabla ya kusafiri hadi Luanda nchini Angola kuvaana na Primeiro de Agosto katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Afrika.


Kama ilivyofanya kwa Wamalawi, Simba ya Mgunda ikaikandamiza Agosto mabao 3-1 na kuifanya icheze mechi tano za kimashindano na mbili za kirafiki na kushinda zote ikifunga jumla ya mabao 15, yakiwamo 11 ya kimashindano na kuruhusu bao moja pekee dhidi ya Agosto.


Rekodi hizo zilimfanya kocha huyo kuwafunika baadhi ya makocha wa kigeni kama vile Pablo Franco, Zoran Maki, Didier Gomes, Sven Vandenbroeck na hata Patrick Aussems ambaye kwa sasa anaifundisha Singida Black Stars. 


TAKWIMU ZAKE


Ndani ya msimu wake wa kwanza kama kocha wa mpito Simba, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyetamba na Coastal Union na kubeba nayo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1988, aliiongoza timu hiyo katika michezo 22, alishinda 17, sare mara nne na kupoteza mara moja tu.


Aliiongoza Simba kufunga mabao 52, huku kikosi chake kiliruhusu mabao tisa tu. Huyo ndiye Mgunda ambaye mwenye anakiri namna ambavyo aliyekuwa msaidizi wake, Seleman Matola alivyoifanya kazi yake kuwa rahisi.


“Niliingia Simba na kwa bahati nzuri nilikutana na Matola, huko nyuma nimewahi kufanya naye kazi hivyo ilikuwa rahisi kwangu kufanikisha mipango ya timu kwa pamoja,” anasema kocha huyo.


Kwa mujibu wa takwimu, Simba ya Mgunda ilikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 77.27, ilitoa mwelekeo mzuri kiasi wadau wengi wakaanza kumpigia debe kuwa anatosha kupewa kibarua cha moja kwa moja lakini haikuwa hivyo kwani mabosi wa klabu hiyo wa Msimbazi walimuajiri kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.


ALIVYOWEKWA KANDO

Simba ilihitaji kuanza zama mpya ikiwa na benchi jipya la ufundi hivyo Mgunda ilibidi kuwekwa kando licha ya kwamba bado alikuwa na mkataba na timu hiyo.

Haikuwa shida kwa kocha huyo, ni kama alikuwa mchezaji wa akiba ambaye alikuwa akipasha pembeni, alianza kutumika katika timu za vijana hasa wakati ambao Simba ilianza kukisuka upya kikosi chao kwa kuingia mtaani.


Kocha huyo alishirikiana kwa karibu na Patrick Rweyemamu ambaye alibeba maono ya kusaka kina Said Ndemla, Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude wengine ambao wanaweza kuwa msaada kwenye kikosi hicho kwa miaka michache ijayo


Baada ya kukamilika kwa kazi kubwa ambayo naye alishiriki, kikosi hicho kilisalia mikononi mwa Rweyemamu ambaye kwa sasa amerejeshwa katika nafasi yake ya meneja wa kikosi cha kwanza, alikokuwa akishirikiana na John Bocco kabla ya straika huyo aliyejulika pia kwa jina la utani la ‘Adebayor’ kutimkia zake JKT Tanzania aliko sasa.


Mgunda aliongeza nguvu upande wa timu ya wanawake ya Simba Queens ambako alikuwepo Mussa Hassan Mgosi.


SIMBA YAMRUDISHA

Baada ya kubwaga manyanga kwa Abdelhak Benchikha mwishoni mwa msimu uliopita, viongozi wa Simba hawakuwa na namna ilibidi warudi kwa Mgunda na kumbebesha zigo la kumalizia michezo iliyosalia huku wao wakiendelea na taribu za kusaka mrithi wa Mualgeria huyo.


Mgunda akishirikiana na Matola kwa mara nyingine tena, waliiongoza timu hiyo katika mazingira magumu, kivipi? Tayari kulikuwa na utofauti mkubwa wa pointi baina yao na Yanga ambao walikuwa wakiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, hivyo mpango ukasalia kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kati yao na Azam FC.


Huku akiwakosa baadhi ya wachezaji muhimu ambao walizoeleka katika kikosi cha kwanza, aliwaibua kina Edwin Balua, Ladack Chasambi na Salehe Karabaka na kuifanya Simba kushika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC na kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.


GAMONDI ALIZIDIWA

Kuonyesha na kutambua ukubwa wa kazi ambayo aliifanya Mgunda katika kipindi cha mwezi Mei akiwa na kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi, Kamati ya tuzo za Ligi Kuu Bara ilimchagua kuwa mshindi wa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu wa mwezi Mei.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mgunda aliwapiku, Miguel Gamondi wa Yanga na Bruno Ferry wa Azam ambao alikuwa anashindana nao kuwania tuzo hiyo.


Ndani ya kipindi cha mwezi Mei, Mgunda aliiwezesha Simba kushinda mechi sita kati ya saba walizocheza na kukusanya pointi 19.

Mechi hizo ni dhidi ya Mtibwa (2-0), Tabora United (2-0), Azam FC (3-0), Geita Gold (4-1), KMC (1-0), JKT Tanzania (2-0), Kagera Sugar (1-1).


SIMBA QUEENS

Kipindi cha mwaka mmoja cha Mgunda kilikuwa na mafanikio makubwa, kwani aliisaidia Simba Queens kurudisha taji la Ligi Kuu, jambo ambalo limeongeza heshima kwa timu hiyo. Uwezo wake wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ulikuwa dhahiri, na uongozi wa Simba ukampongeza kwa utumishi wake wa uadilifu na weledi.


Baada ya kuondoka kwa Mgunda, Simba Queens sasa itakuwa chini ya uongozi wa Mussa Hassan Mgosi, ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu hiyo. Mgosi ameanza rasmi maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya wanawake Tanzania, huku akitazamia kuendeleza mafanikio yaliyowekwa na mtangulizi wake. Kocha Mgosi ni mchezaji wa zamani wa Simba SC, na anaeleweka kuwa na uelewa mkubwa wa soka la ndani na nje ya nchi.


Mabadiliko haya yanakuja wakati ambapo Simba Queens inajiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL), ambapo matumaini ya mashabiki ni kuona timu hiyo ikiendelea kung’ara kama ilivyofanya msimu uliopita. Mgosi tayari amekutana na wachezaji na kuanza maandalizi, lengo likiwa ni kuendeleza utawala wa Simba Queens katika soka la wanawake nchini.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad