Steve Nyerere Hataki Tena ishu za Kuchangisha Rambirambi

 


Ilikuwa jioni kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, baada ya Tamasha la Faraja ya Tasnia lililokuwa linahusu kuwakumbuka wasanii waliotangulia mbele za haki kwa kuwafanyiwa dua.


Tamasha hilo liliandaliwa na Steve Nyerere ni moja ya mambo makubwa anayoyafanya kwenye tasnia ya filamu akiwa pia ni mchekeshaji wa Bongo Movies na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao.


Mwanaspoti kama kawaida lilipata wasaa wa kuongea naye kwenye ‘Dakika 5 na...’ na amefunguka machache ikiwamo kuwashukuru waliofika kwenye tamasha hilo.


Tamasha la Faraja lilifana;


“Nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliofika katika Tamasha hili la Faraja ya Tasnia, hata wale ambao hawakuweza kufika ila walikuwa wanafuatilia ‘live’ kwenye media. Pia nawashakuru sana. Na nikwambie tu mimi ni mtu na nusu na naiamini na kujiweza kwenye utendaji wa jambo langu na hata la wengine.”


Pia amesema hajakata tamaa ya kugombea nafasi ya Ubunge japo alishagombea mara tatu kupitia Chama Cha Mapinduzi na kushindwa kwenye kura za maoni.


“Nikwambie tu kitu kimoja nilihairisha kugombea Ubunge baada ya kushindwa mara kadhaa, sasa nimeamua kuwa na nia hiyo, uwezo ninao na nia ninayo na utendaji ninao wa kutosha.”


Kaibukia kwenye taasisi, vipi sanaa?


Hapana mimi bado ni muigizaji, nembo ya uigizaji haijatoka bado, sababu ni utambulisho wangu huu. Ila nimeona kujiongeza sababu mimi nina uwezo wa kufanya kitu chochote chenye kuleta tija, chenye kuleta matokeo mazuri, sio hayo tu hata kwenye siasa mimi ni zaidi ya mwanasiasa na najua ninachokifanya, ndiyo maana mimi sifa yangu kubwa ni kujiamini.


Unaiona wapi sanaa ya sasa?


Tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani, sanaa ya Tanzania imepanda juu sana, namaanisha sekta zote za burudani, kuanzia soka, muziki na uigizaji hivyo kilichobakia ni sisi wahusika kufanya biashara na kumwonyesha Mama Samia kwa vitendo kile alichowekeza kwetu kinafanyiwa kazi.


Sitaki tena mambo ya misiba


Nimegundua kuna watu baadhi wanaonizunguka ni wanafiki, walikuwa karibu na mimi kwa lengo la kunichafua, yaani haiwezekani kitu wanafahamu kabisa mlolongo mzima wa michango ya rambirambi za misiba niliyokuwa nasimamia halafu baada ya hapo wanakuja kutangaza nimepiga pesa hii kitu ni mbaya sana ni unafiki uliofika kikomo


Hii narudia tena nilishaliongea wenye kuelewa walinielewa na wasionielewa siwalazimishi wanielewe, ila watu wanatakiwa kuelewe kwanza mimi huwa sijichagui mimi mwenyewe kuwa mwenyekiti wa kamati za misiba, bali huwa tunakusanyika watu wengi tu na baada ya hapo mimi nachaguliwa na watu kusimamia hilo na hii sababu wameona nina kipaji cha uaminifu.


Sasa wanatokea watu na sera zao ambazo hazina mashiko wanakuja kutangaza mimi mlaji wa pesa za michango ya rambirambi. Na hii wala sifichi watu wenyewe ni hawa hawa wasanii wenzangu ndio huwa wanaanzisha hizi mada baada ya kuona jambo limekwenda vizuri, kiufupi baadhi yetu tuache kuendekeza umaskini ili tuweze kufika mbali.


Kitu kingine watu wasichokijua acha nikwambie ukweli leo kwa kuwa umeniuliza, katika hizo pesa za michango ya rambirambi mimi huwa sishiki pesa, sababu huwa tunateua Mwenyekiti, Katibu na Mwekahazina, sasa mwekahazina yupo mimi nashika pesa za nini? Na hata huyo mwekahazina akitoa pesa lazima watu wote tujulishwe matumizi yake sasa pesa zinapigwaje hapo?


Tabia gani ambazo huzipendi?


Sipendi tabia ya watu kutokupendana, tabia ya kupendana kwa unafki na kupeana sifa za kijinga tena za uongo, tena hasa sisi wasanii asilimia kubwa ya wasanii wanaishi maisha ya kuigiza kama wanavyoigiza kwenye sanaa zetu, mtu ataigiza anakupenda anakukimbilia kwenye shida lakini huamini huyo mtu anakuwa anaigiza na naimani tungekuwa wamoja sisi wasanii tungefika mbali, tatizo majungu na roho mbaya za kusemanasemana.


Mimi napenda kutukanwa, napenda kusemwa sana kwa mambo mabaya, yaani nisipotukanwa siku moja ikipita basi naweza kunywa dawa ya maumivu, napenda kuwa na maadui wengi ili niweze kusonga mbele, sasa nchi hii nisipotukanwa mimi Steve Nyerere atatukanwa nani?. Mimi ndio jalala lao, Kitu kingine mimi napenda kuwa na furaha muda wote.


Wewe ni shabiki wa Timu gani?


Mimi ni Shabiki wa Yanga, ila sihitaji maswali mengi ya kuhusu mpira embu kwenda zako hapa... (Anacheka) Usiniletee balaa lako nikaja kukosea majina ya wachezaji mimi, ila kiufupi Yanga timu bora na mwaka huu naitabiria ushindi mwingine wa ligi inayoendelea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad