Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilipata ushindi ugenini dhidi ya timu ya Taifa ya Guinea mchezo uliofanyika jana, Jumanne, Septemba 10, 2024 kwenye uwanja wa Charles Konan Banny, Yamoussoukro, Ivory Coast.
Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inashika nafasi ya sita kwenye orodha ya Ligi Bora Afrika kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na shirika la IFFHS, ilithibitishwa ubora wake baada ya Taifa Stars kuwatumia wachezaji wengi wanaotumikia klabu zake tofauti na kuwasimamisha wachezaji wa Guinea ambao wanacheza soka la kulipwa katika Ligi mbalimbali Ulaya.
Stars ilipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Guinea, huku ikiingia na wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza wanaokipiga ligi kuu Tanzania Bara, kasoro Novatus Miroshi anayekipiga Ligi kuu ya Uturuki.
Timu ya Guinea iliingia na wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza wote wakiwa wanacheza Ligi mbalimbali Ulaya.
Guinea ilianza kupata bao dakika ya 57 kupitia mshambuliaji wao hatari Mohamed Bayo anayekipiga kwenye Klabu ya Lille ya League One, Ufaransa, lakini iliwachukua dakika nne Taifa Stars kurudisha bao kupitia kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuachia shuti kali ambalo lilimshinda mlinda mlango Ibrahim Kone na kuingia wavuni.
Stars iliendelea kucheza kwa tahadhari kubwa, huku ikifanya mashambulizi ya kushitukiza ambapo dakika ya 88, Mudathir Yahya alifunga bao la pili akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Guinea, Ibrahim Kone baada ya shuti la Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Hadi mchezo huo unamalizika Stars iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 ikipanda mpaka nafasi ya pili kwenye kundi H ikiwa na pointi nne huku vinara wakiwa ni DR Congo wenye pointi sita, Ethiopia nafasi ya tatu wakiwa na pointi moja wakati Guinea wakiwa wa mwisho bila pointi.
Wachezaji wengine kutoka Ligi kuu waliyoenda kuwakilisha mataifa yao ni Clatous Chama aliyecheza kwa dakika 89 na Kennedy Musonda alicheza kwa dakika 90 na kufunga bao katika mchezo baina ya Zambia na Sierra Leone, Prince Dube alicheza kwa dakika 79 katika mchezo baina ya Zimbabwe na Cameroon, Duke Abuya alicheza kwa dakika 90 na kufunga bao kwenye mechi baina ya Namibia dhidi ya Kenya, Djigui Diarra alicheza kwa dakika 90 katika mechi kati ya Eswatini dhidi ya Mali, huku Khalid Aucho akicheza kwa dakika 88 na Steven Mukwala aliyecheza dakika mbili katika mechi ya Uganda na Congo.
Kikosi cha Stars kilichoanza ni Ally Salim (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Mohamed Husseini (Simba), Ibrahim Bacca (Yanga), Dickson Job (Yanga), Mudathir Yahya (Yanga), Feisal Salum (Azam), Novatus Miroshi (Goztepe), Edwin Balua (Simba), Waziri Junior (KMC), na Clement Mzize (Yanga).
Kikosi cha Guinea kilichoanza ni Ibrahim Kone (League 2, Ufaransa), Antoine Conte (Parva Liga, Bulgaria) Ibrahim Diakite (Pro League, Ubeligiji), Ibrahim Conte (Super Liga, Romania), Mohamed Camara (Super League, Uswizi), Abdoulaye Toure (League 1, Ufaransa), Ilaix Moriba (La Liga, Hispania), Aguibou Camara (Parva Liga, Bulgaria), Mady Camara (Super Liga, Ugiriki), Aliou Balde (Bundesliga, Ujerumani), Mohamed Bayo (League 1, Ufaransa).