Tatizo si Kina Makipa Diarra, Camara Bali Kukosa Mipango

 

Tatizo si Kina Makipa Diarra, Camara Bali Kukosa Mipango

Wakati klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inausaka ufalme wa soka Afrika, ilimuona Mbwana Samatta kama mmoja wa wachezaji wanaoeweza kusaidia kufanikisha ndoto hiyo.


Hawakusita na kuamua kumchukua wakiwa wamekuja na fedha mbele. Samatta akawa Mtanzania wa kwanza kutwaa taji hilo akiwa na wababe hao wa Lubumbashi.

Mazembe pia walirudi nchini kumchukua Thomas Ulimwengu, wapo Wamorocco waliomfuata Simon Msuva, wako waliomfuata Himid Mao na Watanzania wengine kadhaa.


Na hivi sasa Wamorocco wamekuja kwa nguvu kumtaka mshambuliaji anayeibukia wa Tanzania, Clement Msuva wakimuona kama mmoja wa washnambuliaji wanaoweza kufanikisha ndoto yao ya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya nne tangu klabu hiyo ianzishwe.


Na ili kuionyesha kuwa nia yao ni ya dhati wametanguliza dau la dola 500,000 linaloambatana na posho kadhaa zikiwemo za kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika.


Wapo washambuliaji, viungo na mabeki waliofuatwa na timu za nje kwa ajili ya kwenda kusaidia kufikia ndoto zao, huku baadhi wakifanikiwa na wengine kufikia viwango vya juu vya matarajio yao, huku wengine wakiboronga kabisa baada ya timu zao kushuka.


Mara nyingi, timu hutafuta mchezaji kulingana na uwezo wake wa wakati huo, mahitaji ya timu kwenye nafasi fulani, ama kuongeza wigo wa kocha kuchagua (kikosi kipana) ama sababu nyingine za kimpira.


Kwa bahati, timu zilizokuja hapa zimemfuata washambuliaji viungo na mabeki. Wapo akina Yusuf Macho, Ali Shah, Bakari Malima, Abdul Banda, Singano, Messi, Samatta, Ulimwengu, Mao, Renatus Njohole, Msuva na wengine wengi ambao waliwahi kwenda nje kusakata soka.


Lakini imekuwa ni nadra sana kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya kipa kufuatwa kwa nguvu kiasi hicho. Yupo Idd  Pazi ambaye alikwenda hadi Indonesia kucheza soka la kulipwa. Pia alicheza Sudan na Afrika Kusini.


Ni kati ya makipa wachache wazawa kuchukuliwa na timu za nje, lakini mara nyingi chaguo la kwanza kwa timu za nje huwa ni washamnbuliaji, baadaye viungo na kwa nadra mabeki.


Lakini tumekuwa na makipa bora tangu zamani. Kipa kama Omary Mahadhi aliwahi kutangazwa kwenye kikosi bora cha Afrika, wakati Athuman Mambosasa, Aishi Manula, Juma Kaseja, Hamisi Kinye, Juma Pondamali 'Mensah' na Mohamed Mwameja wamekuwa na ubora wa juu kwa nyakati tofauti, wala wasitamaniwe na klabu kubwa za nje.


Kwa hiyo, ule mjadala kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liangalie uwezekano wa kuzuia makipa kutoka nje kusajiliwa na klabu za Tanzania ili tuilinde nafasi hiyo, haujaangalia sana historia ya wachezaji wetu kwenda nje au mwenendo wa dunia kwa sasa.


Kutosajili makipa wageni kunaweza kusisaidie kabisa makipa wazawa kuongeza viwango vyao na kuonekana ili wachukuliwe na klabu za nje. Kwa kuangalia orodha ya makipa nhyota wazawa ya hapo awali, utabaini kuwa klabu kama Simba imekuwa ikitumia makipa wazawa mara nyingi sana na hivyo kuonekana hata katika ngazi za juu za mashindano makubwa Afrika.


Kwa miaka mine mfululizo, Aishi Manula amekuwa langoni mwa Simba wakagti klabu hiyo ikifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Mwameja ndio aliipeleka Simba fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, huku Mahadhi akiifikisha Simba robo fainali mwaka 1974. Hakuna hata mmoja kati yao aliyetamanisha klabu vigogo Afrika.


Na makipa hao wamecheza kikosi cha kwanza Simba na timu ya taifa, Taifa Stars bila ya kuwa na kanuni yoyote ya kuzuia makipa wageni. Ni miaka ya karibuni tu ndio klabu zinazoiwakilisha Tanzania zilipoanza kusajili hata makipa kutoka nje.


Kwa hiyo hoja si kuzuia makipa wageni ili wazawa waonyeshe vipaji au kwa sababu tuna makipa wazuri wengi, bali uzuri wao unalingana na viwango ambavyo mpira wa sasa unavitaka. Kwa sababu kama ni kupata nafasi walishapata nafasi sana na kama ni kuonyesha ubora wao wqalishaonyesha sana na kama ni uwezo wao kukubalika hapa nchini, ulishakubalika sana.


Lakini tunaona mageuzi katika makipa wa kisasa wanaosajiliwa na klabu zetu. Bila ya shaka, jina la kwanza linakuja la Djigui Diarra ambaye amekuwa kioo cha makipa wengi wazawa, na wengi wanaona haja ya kufanya vitu vingi Zaidi ya kusubiri michomo golini.


Na kipa mpya wa Simba, Camara amepigilia msumari kuwa mpira wa sasa unahitaji kipa anayefanya mambo mengi Zaidi ya kusubiri mikwaju na krosi golini kwake.


Kwa hiyo badala ya kufunga milango kwa makipa wageni, ni muhimu kufikiria mkakati wa kutengeneza makipa wa sasa wanaohitajiwa na soka la sasa. Na hii itawezaekana kwa kuzalisha makocha wengi zaidi wa eneo hilo na kuwa na mafunzo ya mara kwa mara ya kuboresha stadi za ukipa.


Makipa wetu hawawezi kuongeza ubora kwa sababu ya kuwaona akina Diarra na Camara, bali kwa kupata mafunzo sahihi kuanzia katika umri mdogo kabisa. Na hilo litawezekana kama ukiwa na walimu sahihi katika soka la watoto.


Tusifikirie hatua kali zinazoangalia tulipoangukia, bali tuwe na mtazamo mpana unaoangalia tulipojikwaa, bila ya hivyo tutakuwa tunarekebisha matokeo ya tatizo na si chanzo cha tatizo.


Diarra na Camara walipikwa na ndio maana wanakubalika katika soka la sasa, nasi tuinghie jikoni tuwapike hata kama mapishi hayo yatachukua muda mrefu, ili mradi tu mwishoni uonekane mwanga.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad