Kuna kitu kinakwenda kutokea usiku wa leo pale Amaan Zanzibar. Azam inakwenda kuikaribisha Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo kiufundi utamu uko pale kati kwenye kiungo.
Katika mechi kadhaa zilizopita timu hizo zimekuwa na ufanisi mkubwa kwenye eneo hilo kutokana na aina ya mastaa waliosajiliwa.
Azam chini ya Fei Toto, Adolf Mtasingwa, James Akaminko, Ever Meza na wengineo, imekuwa ikicheza soka la kuvutia ingawa kwenye mechi kadhaa imekosa matokeo tarajiwa.
Lakini dhidi ya Simba leo huenda ikawa stori nyingine kwani ushindani huwa ni mkubwa zaidi huku wachezaji wakipania kuonyeshana undava. Pale kati Simba nako gari limewaka haswa kutokana na ubora walioonyesha kwenye mechi mbili za CAF. Yupo Yusuph Kagoma, Jean Charles Ahua halafu unamalizia na fundi Debora Mavambo ambaye amewaka kwa kuonyesha ubora ambao umekuwa gumzo midomoni mwa mashabiki wanaoamini kwamba leo saa 2:30 usiku pale kati kitawaka.
Ni pambano lenye mvuto na msisimko wa aina yake kutokana na ushindani uliopo baina ya timu hizo tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008.
Mwanaspoti linakuletea rekodi kadhaa za michezo 32 ya ligi baina ya timu hizo tangu msimu wa 2008-2009, pale Azam ilipopanda daraja.
Zinakutana huku vikosi vyote viwili vikiwa chini ya makocha wapya, Azam ikiwa na Mmorocco Rachid Taoussi na Simba ina Msauzi, Fadlu Davids wanaokutana kwa mara ya kwanza katika Bara, lakini zote zikiwa na wachezaji mahiri na wote wapo Unguja.
SIMBA MBABE
Katika michezo 32 iliyochezwa baina ya timu hizo, Simba ndio wanaoonekana kuwa wababe zaidi mbele ya Azam kwa takwimu mbalimbali.
Simba imeshinda michezo mingi zaidi mbele ya Azam, ikifanya hivyo mara 14 dhidi ya sita tu ya Wanalambalamba, huku ikiongoza pia kwa idadi ya mabao ya kufunga ikiwa na 44 dhidi ya 29 ya wenyeji wa mchezo wa usiku wa leo pale Amaan.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zimeshindwa kutambiana katika mechi 12 iliyoisha kwa sare tofauti, huku Simba ikivuna jumla ya pointi 54 katika michezo yote 32 dhidi ya 30 za wapinzani wao hao ambao msimu uliopita walichezea kichapo cha mabao 3-0 zilipokutana katika mchezo wa mwisho.
Simba imepoteza mechi nne ikiwa nyumbani, huku ikitoka sare tano ikiwa wenyeji, wakati ni mechi mbili tu ndizo ilizopoteza ikiwa ugenini na kutoka sare saba ikicheza huko.
Hali ni tofauti kwa Azam kwani imepoteza michezo saba nyumbani sawa na ile iliyopoteza ugenini na pia kupata sare wakiwa wenyeji, ilihali imeambulia sare tano ugenini mbele ya Simba.
Pambano la leo linakuwa la tatu kwa timu hizo katika Ligi Kuu kukutana nje ya Dar es Salaam baada ya lile la Sept 11, 2010 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, uliotumiwa kama Uwanja wa nyumbani wa Azam na timu hiyo kulala 2-1 mbele ya Mnyama.
Mechi nyingine iliyopigwa nje ya Dar ni ile ya msimu uliopita lililochezwa Februari 9 mwaka huu ambapo Simba ikiwa wenyeji waliupeleka CCM Kirumba, jijini Mwanza na kumalizika kwa sare ya 1-1, Mnyama ikichomoa dakika za lala salama bao la Prince Dube kupitia Clatous Chama.
Kitu cha kuvutia ni kwamba nyota hao waliofunga mabao katika pambano hilo la jijini Mwanza kwa sasa hawapo Msimbazi, kwani wote wamehamia Yanga msimu huu na wikiendi iliyopita walikuwa Uwanja wa Amaan kuisambaratisha CBE SA ya Ethiopia katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu hiyo kutinga makundi.
UNAKUMBUKA HII?
Pambano moja tu baina ya timu hizo katika Ligi Kuu liliwahi kulazwa kiporo na kulazimika kuchezwa siku mbili, likiwa ni ule uliopigwa Mar 30, 2009, ambapo kwanza ulipigwa siku moja na kushindwa kumalizika kutokana na mvua kubwa na kurudiwa kesho yake na Azam iliyokuwa wenyeji wa mchezo huo wa marudiano kwa msimu wa 2008-2009 ikalala mabao 3-0.
MABAO 73
Katika mechi hizo 32 zilizopigwa hadi sasa wanaume hao wamezalisha jumla ya mabao 73, ikiwa ni wastani wa kila mechi moja kuzalisha mabao 2.28, huku Simba ikiongoza kwa kufunga maba0 44 ikiwa ni wastani wa kufunga mabao 1.38 kwa kila mchezo, huku Azam yenye mabao 29 ikiwa na wastani wa 0.9 ya bao kwa kila mechi hizo 32 ilizocheza hadi sasa.
Ni mapambano mawili tu yaliyowahi kuzalisha mabao mengi kwa kila dakika 90, likiwamo lile la Januari 23, 2011 ambapo Simba iliifunga Azam kwa mabao 3-2, kisha Azam nayo ikaja kufanya kama hivyo Machi 4, 2020 ilipoichapa Simba pia kwa mabao 3-2.
NA HII JE?
Ni msimu mmoja tu wa 2017-2018 uliozalisha idadi ndogo ya mabao kwa kufungwa bao moja wakati Simba iliposhinda bao 1-0 katika mechi ya marudiano huku ile ya kwanza ikiisha kwa suluhu, ilihali msimu wa 2010-2011 na ule wa 2012-2013 ndio pekee iliyozalisha mabao mengi kwani kila moja ulishuhudiwa yakifungwa mabao manane kupitia mechi mbili za kila msimu.
WALIOJIFUNGA
Na wachezaji wawili pekee waliowahi kujifunga katika michezo hiyo 32 iliyopita kwa timu hizo katika Ligi, wote wakiwa ni mabeki wa kati wa Azam, akianza Agrey Morris Machi 14, 2010 wkati Azam ikilala kwa mabao 2-0, kisha akafuata Abdallah Kheri ‘Sebo’ Februari 21, mwaka jana wakati akiisawazishia Simba bao dakika ya 90 katika harakati za kuokoa shuti la Kibu Denis.
WAKALI WA REKODI
Rekodi zinaonyesha kuwa, Winga wa zamani wa kimataifa aliyewahi kukipiga katika hizo mbili, Jamal Mnyate ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika Dabi ya Mzizima.
Mnyate alifunga bao katika pambano la kwanza kwa timu hizo msimu wa 2008-2009 mchezo uliochezwa Oktoba 4, 2008 ambapo Simba ilicharazwa nyumbani mabao 2-0. Mnyate enzi hizo akiwa Azam alifunga katika dakika ya 42 kabla ya Shekhan Rashid aliyewahi pia kuichezea Simba, kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 90+5 na kuwapa Wanalambalamba ushindi huo mtamu.
Rekodi zinaonyesha pia, Mkenya Mike Barasa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika pambano moja baina ya timu hizo akifanya hivyo katika mechi ya Machi 14, 2010 wakati Simba ikishinda ugenini mabao 2-0.
Ukiachana na rekodi hizo, nahodha aliwahi kuziongoza timu hizo kwa vipindi tofauti, John Bocco ‘Adebayor’ ndiye anayeongoza orodha ya kufunga mabao mengi zaidi, akitupia mabao manane, akifunga sita kipindi akiwa Azam na kuongeza mawili alipokuwa Simba iliyomtema msimu huu.
MK 14, Meddie Kagere aliyekuwa Simba anafuata kwa kufunga jumla ya mabao matano, akiwa ndiye mchezaji aliyeitesa Azam kwa miaka ya karibuni kwa kufunga mfululizo, akifuatiwa na Kipre Tchetche aliyefunga mabao manne enzi akiichezea Azam hadi anaondoka.
Prince Dube aliyepo Yanga kwa sasa ndiye anayefuata akiwa na mabao matatu akifuata nyayo za Kagere za kufunga mfululizo timu pinzani.
MSIMU HUU VIPI?
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu, huku kila moja ikiwa chini ya kocha mpya na sura za wachezaji tofauti ambao wamepewa nafasi kubwa ya kuamua matokeo ya mchezo huo wa visiwani Zanzibar.
Kocha Fadlu Davids wa Simba aliyeanza kwa kishindo msimu wa Ligi Kuu kwa kushinda michezo miwili mfululizo akianza kwa kuinyoa Tabora United kwa mabao 3-0 kisha kuilaza Fountain Gate kwa mabao 4-0 ataendelea kuwategemea Valentino Mashaka, Charles Ahoua wanaoongoza kwa mabao na asisti katika kikosi hicho.
Mashaka aliyesajiliwa msimu huu akitokea Geita Gold anaongoza kikosini akiwa na mabao mawili, huku Ahoua anayetokea Ivory Coast ana bao moja na asisti tatu akiwa ndiye kinara hadi sasa wa ligi hiyo, huku wakitarajiwa kusaidiana na kina Lionel Ateba, Edwin Balua, Steven Mukwala na Joshua Mutale waliotua Msimbazi msimu huu kuisumbua ngome ya Azam chini ya Yeison Fuentes, Yoro Diaby na viungo wanaojua soka, James Akaminko, Adolf Mtasingwa na Ever Meza.
Hata hivyo, Azam sio timu ya kubezwa, kwani katika mechi tatu ilizocheza chini ya kocha mpya, Rachid Taoussi, imevuna pointi saba na mabao matano, huku wavu wake ukiwa haujaguswa.
Ilianza na suluhu na Pamba Jiji kabla ya kuisulubu KMC kwa mabao 4-0 kisha juzi kati kuichapa Coastal Union kwa bao 1-0 na kuifanya ifikishe pointi nane kupitia mechi nne ilizocheza hadi sasa.
Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu iliyopita mbele ya Simba iliyokamata nafasi ya tatu, ilianza msimu huu kwa suluhu na JKT Tanzania ugenini na leo itaendelea kumtegemea kiungo mshambuliaji wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Paschal Msindo aliyehamishiwa eneo la mbele kwa sasa, Idd Selemen ‘Nado’, Nassoro Saadun mwenye mabao mawili kwa sasa na Jhonier Blanco kuisumbua ngome ya Simba chini ya Che Fondoh Malone na Abdulrazak Hamza na viungo Debora Mavambo na Fabrice Ngoma.
Kitu kinachoweza kuiangusha Azam kwa leo ni eneo la kipa, Zubeir Foba sio mzoefu mkubwa kulinganisha na wale wa Simba, akianza Mousa Camara, Aishi Manula au Ally Salim, kutokana na kuumia kwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Mustafa Mohammed aliyekosa mechi tatu zilizopita ambazo hata hivyo, Foba alijitahidi na kutoka na clean sheet mfululizo.
Kwa kuangalia vikosi vilivyo, ni wazi Simba ana nafasi kubwa ya kuendeleza ubabe mbele ya Azam, japo soka huwa na matokeo ya kustaajabisha, hasa ikizingatiwa Azam ikicheza visiwani Zanzibar imekuwa na kismati mbele ya Mnyama, lakini yote kwa yote dakika 90 ndizo zitakazoamua mchezo.
MAKOCHA WANASEMAJE?
Kocha wa Azam, Taoussi alisema; “Ni mchezo muhimu kushinda kwa sababu utatafanya tupande nafasi katika msimamo wa ligi. Tumefanya maandalizi na wachezaji wapo katika ari nzuri. Mazingira ni rafiki hapa. Endapo wachezaji watacheza kama vile ambavyo tumefanyia mazoezi basi naamini tutaondoka na ushindi.”
Fadlu Davids wa Simba kwa upande wake alisema; “Tunakwenda kucheza mechi yetu ya tatu ya ligi dhidi yam pinzani mgumu, tunafahamu umuhimu wa mchezo huo hivyo tumejiandaa vizuri.”
“Tumekuwa na siku mbili za mazoezi tangu tutoke katika mchezo wetu wa mwisho, nina wachezaji wengi ambao wanaweza kufanya vizuri katika mchezo huu bila ya kujali nani amekosekana,” alisema Fadlu.
Vikosi vinavyoweza kuanza leo:
AZAM: Foba, Lusajo, Chilambo, Fuentes, Yoro, Mtasingwa, Akaminko, Msindo, Saadun, Fei Toto na Idd Nado.
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Hamza, Che Malone, Kagoma, Kibu, Debora, Ateba, Ahoua na Mutale.