UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa hawana hofu na wapinzani wao kwenye mchezo wao wa Mzizima Dabi ambao unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Simba imecheza mechi mbili ndani ya Ligi Kuu Bara ambazo ni dakika 180 na kupata ushindi kwenye mechi zote hizo huku Azam FC ikicheza mechi nne ambazo ni dakika 360, ushindi ni kwenye mechi mbili na iliambulia sare kwenye mechi mbili.
Mchezo uliopita kwa Azam FC ilikuwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex baada ya dakika 90 ubao ulisoma Azam FC 1- Coastal Union, hivyo walikomba pointi tatu kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya ule wa kwanza kupata ushindi dhidi ya KMC wa mabao 4-0 uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa hawana hofu na wapinzani wao Azam FC kikubwa ni utayari na wanahitaji pointi tatu muhimu. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Septemba 26 2024.
“Tunakwenda kwenye mchezo wetu tukiwa na ari ya kutafuta ushindi hatuna hofu kuwakabili wapinzani wetu Azam FC ni timu nzuri lakini tunakwenda kukabiliana nao ili kupata pointi tatu muhimu.”