KAMA wewe ni shabiki wa Yanga ambaye popote ilipo timu hiyo nawe unakuwepo, basi anza kujipanga mapema kwani kuna mabadiliko ambayo yataifanya klabu hiyo kuendana na baraka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia.
Yanga ni moja kati ya timu mbili za Tanzania zilizosalia katika michuano ya CAF ikitinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuing’oa Vital’O ya Burundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 10-0 na sasa imepangwa kucheza na CBE ili kusaka tiketi ya kutinga makundi. Timu nyingine ni Simba iliyoanzia hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kucheza na Al Ahli Tripoli ya Libya.
Mara baada ya kujua itavaana na Wahabeshi wakianzia kwanza ugenini kabla ya kurudiana nao baadaye mwezi huu, mabosi wa Yanga fasta walituma maombi CAF wakiomba mchezo huo dhidi ya CBE ukapigwe kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kati ya Septemba 20-22.
Hata hivyo, ghafla zikasambaa taarifa kwamba isingekuwa rahisi kwa mechi hiyo kupigwa huko kwa vile eti uwanja huo umezuiwa na CAF, kabla ya Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) kukanusha uvushi huo na kutoa ufafanuzi kwamba New Amaan umepata baraka zote za kutumika kwa mechi zote za awali za michuano hiyo ya Afrika kwa ngazi ya klabu.
Kabla ya ufafanuzi huo wa ZFF katika taarifa yao ya Agosti 28 mwaka huu iliyosainiwa na Ofisa Habari wake, Mohamed Kabwanga, mapema Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ndiye aliyeweka wazi maombi yao hayo ya mechi ya marudiano mara baada ya kuvaana na wapinzani wao Septemba 13 kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa huko Ethiopia.
Lakini jana, Mwanaspoti ilipenyezewa taarifa kwamba kila kitu kimekaa sawa na Yanga itaenda Zenji kurudiana na Wahabeshi na mshindi wa jumla atatinga makundi, ambayo msimu uliopita timu hiyo ilitinga baada ya miaka 25 kupita na mwishowe kwenda kutolewa kiutata katika robo fainali na Mamelodi Sundown ya Sauzi.
“Mchezo wa marudiano wa Yanga na CBE utachezwa Zanzibar, lakini mtatangaziwa,” chanzo hicho kililidokeza Mwanaspoti, lililoamua kumtafuta Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada aliyethibitisha kwamba CAF tayari imeshatoa baraka zake kwa kuupitisha uwanja huo kuchezewa mechi hiyo.
Ahmada alisema tayari ZFF na wadau wake wameshaanza maandalizi ya kuupokea mchezo huo ambao utatoa hatma ya Yanga katika kusaka rekodi ya kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.
“Ni kweli CAF wameshatujulisha kwamba huu mchezo utatumika kwenye uwanja wetu wa New Amaan kama ambavyo timu mwenyeji wa mchezo huo Yanga walivyoomba,” alisema Ahmada na kuongeza;
“Sisi kama ZFF kwanza tunawashukuru Yanga kwa uamuzi huo wa kizalendo, Zanzibar ni sehemu ambayo ina mashabiki wengi lakini pia hata wale ambao watatoka bara hapa ni rahisi kufika. Hivyo sisi kama ZFF tumeshaanza maandalizi kwa haraka, kujiandaa na kupokea wageni kwa timu zote lakini pia mashabiki wao tunaamini Uwanja wa Amaan utakuwa ni baraka kwa Yanga kushinda kwa kishindo na hata kufuzu kuingia makundi na pengine kwenda mbali zaidi.”
Tangu uwanja huo ukarabatiwe, Yanga iliugusa mara ya mwisho kwa mafanikio ilipotwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kuinyoosha Azam kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu katika fainali kali iliyopigwa Juni 3,2024.
Kwenda kucheza mchezo huo visiwani humo, haitaiathiri Yanga kwani tayari mechi mbili za awali za raundi ya kwanza dhidi ya Vital’O ya Burundi zilichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex pia ni wa nyasi bandia kama ulivyo Amaan uliotumiwa jana kwa fainali ya Ngao ya Jamii kati ya JKU na Chipukizi.