Yanga Wafunguka: Tutawamaliza Waethiopia huko huko kwao

 

Yanga Wafunguka: Tutawamaliza Waethiopia huko huko kwao

Licha ya kubakia na wachezaji wachache kambini, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameendelea na programu yake kwa ajili ya kujiandaa kuwakabili CBE ya Ethiopia katika mchezo wa raundi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


CBE watawakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Abebe Bikila ulioko jijini Addis huku mechi ya marudiano ikitarajiwa kufanyika wiki moja baadaye kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Hata hivyo Gamondi ameanza mazoezi akiwa na wachezaji 11 tu kutokana na nyota wengine kuitwa katika majukumu ya kimataifa.


Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, aliliambia gazeti hili Gamondi anaendelea na programu yake kwa sababu anataka wachezaji waliobakia pia kuwa fiti na tayari kwa mchezo huo wa ugenini.


Alisema wanafahamu mchezo huo hautakuwa rahisi na ndio sababu wameanza mapema mazoezi kwa sababu wanataka kwenda kuvuna matokeo mazuri ugenini.


"Yanga imesajili wachezaji 27, kati ya hao 14 wamekwenda kuziwakilisha nchi zao katika michezo wa kimataifa, wengine wameitwa Taifa Stars, Mali, Burkina Faso, Zambia, Kenya, Uganda na kwingine, tumebakiwa kambini na wachezaji 13 tu na kati ya hao wawili wana majeraha," alisema Kamwe.


Aliongeza pia katika kikosi chao wana wachezaji wawili majeruhi ambao ni Yao Kouassi na Farid Mussa.


"Kwa maana hiyo tumebakiwa na wachezaji 11 tu, lakini mwalimu bado anaendelea na programu yake kama kawaida, amehitaji mchezo mmoja wa kirafiki ili kujipima na kuangalia utimamu wa mwili wa wachezaji wake, anajua wale wengine watarudi wakiwa fiti kwa sababu wanaenda kuzipambania nchi kwa kucheza mechi ngumu," Kamwe alisema.


Aliongeza anakiandaa kikosi chake kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo na tayari wameshaanza 'kuwasoma' wapinzani wao.


"Gamondi alihitaji mchezo wa kirafiki na sisi tukaamua kuwaita wenzetu wa Kiluvya FC tukacheza nao, ilikuwa ni mechi ya kirafiki na ya kimazoezi, haikuwa na shabiki yoyote aliyeruhusiwa kuingia kutazama kwa sababu tulikuwa tumebakiwa na wachezaji 11, tukalazimika kuwaongeza wachezaji watatu wa kikosi cha pili.


Kwa bahati nzuri ulikuwa mchezo mzuri, haukuwa wa kukamiana, tukashinda mabao 3-0, na tunafikiria siku hizi chache zingine tucheze mechi nyingine kama hii, ambapo mwalimu amehitaji tena ili kuwaimarisha nyota wake walioko kabla wale wengine hawajarejea nchini," aliongeza ofisa huyo.


Alisema maandalizi ya safari ya kuelekea  Ethiopia yako katika hatua za mwisho na wanaamini wakiwa ugenini wataendeleza 'moto' waliounza katika mashindano hayo ya kimataifa msimu huu.


Mechi dhidi ya Kiluvya FC ilichezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex na mabao ya Yanga yalifungwa na Shekhan Ibrahim, Salum Aboubakar 'Sure Boy' na Mkongomani Jean Baleke.


Yanga imesonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga Vital'O ya Burundi jumla ya mabao 10-0, katika mechi mbili ambazo zote zilichezwa, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.


Awali iliichapa mabao 4-0, kabla ya kuikandika magoli 6-0 katika mchezo wa mkondo wa pili, ambapo wapinzani wao waliamua kuuchagua Uwanja wa Azam  kutokana na viwanja nchini kwao kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad