KÄ°PA Aishi Salum Manula ndiye mkongwe pekee aliyeitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars cha wachezaji wanaocheza nyumbani pekee kwa ajili ya mechi ya kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Sudan wiki ijayo.
Taifa Stars watakuwa wageni wa Sudan Jumapili ya Oktoba 27 Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya Jijini Nouakchott nchini Mauritania, kabla ya timu hizo kurudiana Jumapili ya Novemba 3 Uwanja Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya Ethiopia na Eritrea mwezi Desemba katika hatua ya mwisho ya mchujo wa tiketi ya CHAN, ingawa Tanzania na Kenya zimekwishafuzu kwa tiketi ya uenyeji.
Kikosi kamili cha Taifa Stars ya CHAN kitakachokuwa chini ya kocha Bakari Nyundo Shime kinaundwa na Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Isaya Kasanga (Tanzania Prisons U17) na Anthony Mpemba (Azam U20).
Mabeki; Paschal Msindo (Azam FC), David Bryson (JKT Tanzania), Nickson Mosha (KMC FC), Lameck Lawi (Coastal Union), Abdulrahij Bausi (JKT Tanzania), Vedastus Masinde (TMA FC) na Ibrahim Ame (Mashujaa FC).
Viungo; Hija Shamte (Kagera Sugar), Adolf Mtasingwa (Azam FC), Abdulkarim Kiswanya (Azam FC U20), Charles Semfuko (Coastal Union), Shekhan Khamis (Yanga), Ahmed Pipino (Magnet FC), Sabri Kondo (KVZ), Salum Ramadhan (Ken Gold), Ismail Kader (JKT Tanzania) na Bakari Msimu (Coastal Union).
Washambuliaji; William Edgar (Fountain Gate), Suleiman Mwalimu (Fountain Gate), Valentino Mashaka (Simba SC) na Crispin Ngushi (Mashujaa FC).