Kufuatia droo ya hatua ya makundi iliyochezeshwa siku ya leo Jumatatu mjini Cairo, Misri, Klabu ya Wekundu wa Msimbazi imetupwa katika kundi A dhidi ya wapinzani wake ambao ni CS Sfaxien ya Tunisia, CS Constantine ya Algeria, na FC Bravos do Maquis ya Angola.
Katika kundi hilo ambalo Simba ilikuwa katika pot 1 iliyokuwa ikijumuisha timu timu zenye alama nyingi za CAF kwa kipindi cha miaka mitano ya nyuma, itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya klabu ya CS Sfaxien na Tunisia ambayo ndio timu inayoongoza kwa kutwaa ubingwa wa kombe la shirikisho Afrika mara nyingi kuliko klabu yeyote.
Klabu hio imefanikiwa kutwaa ubingwa huo mara tatu, mwaka 2007, 2008 pamoja na mwaka 2013 na hadi sasa mwaka 2024 hakuna timu iliyofanikiwa kushinda ubingwa huo mara 3 au zaidi.
Sfaxien katika msimamo wa ligi ya Tunisia inayojulikana kama Tunisia Ligue 1 msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Esperance de Tunis na Etoile du Sahel na katika msimu huu hadi sasa inashika nafasi ya 6 ikiwa na alama 7 katika michezo minne.
Pia Simba itacheza na klabu ya Bravos ya Angola ambayo ndio iliyowaondoa klabu ya Coastal Union ya Tanzania katika hatua ya awali kabisa katika michuano hii.
28.11.2024: Simba vs Bravos
08.12.2024: CS Constantine vs Simba
15.12.2024: Simba vs CS Sfaxien
05.01.2025: CS Sfaxien vs Simba
12.01.2025: Bravos vs Simba
19.01.2025: Simba vs CS Constantine.