Hazard na Salah ni wanasoka mahiri kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England miaka ya karibuni. Hazard alitumikia misimu saba yenye mafanikio kwenye kikosi cha Chelsea, wakati Salah amekuwa mchezaji muhimu kabisa katika timu ya Liverpool.
LIVERPOOL, ENGLAND: SUPASTAA wa zamani wa Chelsea na Real Madrid, Eden Hazard amesema staa wa Liverpool, Mohamed Salah ni mchezaji bora kumzidi yeye kwa kiwango kikubwa sana baada ya wawili hao kuwahi kuwa pamoja Stamford Bridge
Hazard na Salah ni wanasoka mahiri kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England miaka ya karibuni. Hazard alitumikia misimu saba yenye mafanikio kwenye kikosi cha Chelsea, wakati Salah amekuwa mchezaji muhimu kabisa katika timu ya Liverpool.
Hata hivyo, Hazard hakusita kumweka Mo Salah juu yake kwenye ubora, wakati alipoulizwa anadhani ni mchezaji gani bora baina yake, ambapo winga huyo wa zamani wa Ubelgiji, alisema. “Mo Salah, ameniacha mbali sana.”
Wawili hao walicheza pamoja wakati Mo Salah alipokuwa Chelsea, lakini mkali huyo wa kimataifa wa Misri hakupata nafasi za kutosha za kucheza huko Stamford Bridge, hivyo alitolewa kwa mkopo kwenda Italia, alikoenda kuzitumikia Fiorentina na AS Roma.
Baada ya kucheza vyema kwa mkopo, Mo Salah alijiunga jumla AS Roma mwaka 2016 na kisha kusajiliwa na Liverpool msimu uliofuatia baada ya kuichangia timu hiyo ya Serie A mabao 34 katika mechi 41.
Tangu alipojiunga na Liverpool, Salah amefunga mabao 216 katika mechi 357 za michuano yote na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji ya Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA na Kombe la Ligi. Anashika namba sita kwenye orodha ya vinara wa mabao wa muda wote kwenye kikosi cha Liverpool.