Winga wa Simba Joshua Mutale, amesema amefumba macho na kuziba masikio kuhusu watu wanamponda kutokana na kiwango chake kutowaridhisha wengi akisema kuwa akili yake anaelekeza kwenye ufanisi wa kazi iliyomleta ndani ya kikosi cha wekundu hao wa msimbazi.
Ametoa kauli hiyo baada ya kuibuka maneno mengi kutoka kwa mashabiki wakimlaumu kuwa na mambo mengi uwanjani kitu ambacho wanaamini kinaigharimu timu yao na kushindwa kupata mabao mengi.
Mutale ameliambia Spotileo kuwa kukosolewa ni sehemu ya mpira wa miguu na mtu yeyote ambaye anahitaji kujifunza au kuwa bora hawezi kuchukia kukosolewa na badala yake anatafuta njia ya kurekebisha makosa.
“Kukosolewa ni sehemu ya mpira wa miguu. siwezi kuchukia kukosolewa, nachukulia kama sehemu ya kunijenga ili niwe bora, najua haiwezekani nikapendwa na wote, nitapambana kuhakikisha nawapa furaha kila wakati kwani malengo ya Simba ni kushinda vikombe kila msimu.
Uzuri ninajua kilichonileta Simba, ninahitaji kuzifanyia kazi changamoto zote zinazokuja mbele yangu ili kuhakikisha ninafanya vizuri na kuisaidia timu yangu msimu huu ambao umebeba matumaini makubwa kwetu na kwa mashabiki,” amesema Mutale.
Baada ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, amesema anaamini wanayo nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kufika fainali kama sio kutwaa kabisa ubingwa huo.