Akizungumza jijini Dar es Saaam jana, raia huyo wa Afrika Kusini, alisema licha ya kwamba tayari atakuwa ameshaongeza wachezaji kipindi cha usajili wa dirisha dogo, lakini kitaalamu, atakuwa ameshakinoa kikosi hicho kwa muda wa miezi sita huku kikiwa kinapambana uwanjani.
"Kitaalamu ni kwamba klabu yoyote inaposajili kiasi cha wachezaji 15 na kocha mpya inatakiwa miezi sita ili kuona kiwango halisi cha timu na muunganiko wa wachezaji, kwani watakuwa wameshaelewana mikimbio, mifumo, sifa na udhaifu wa kila mchezaji ili kusaidiana uwanjani, tulianza ligi na michuano ya kimataifa Agosti, tukiwa na kikosi kichanga kinachojengwa, kipindi hiki tunamalizia ujenzi, lakini mabadiliko yanaonekana," alisema kocha huyo.
Alisema kwa michezo minane ya Ligi Kuu ambayo timu yake imecheza mpaka sasa, na miwili ya Kombe la Shirikisho, inaonekana inapiga hatua, lakini bado mpaka Februari mwakani ndipo kikosi hicho kitakuwa kimeshakamilika vile inavyotakiwa kitaalamu.
"Kuna mabadiliko makubwa sana kwenye kikosi changu, unaweza kuona sasa baadhi ya wachezaji wameanza kuelewana na wenzao, wanaweza kupiga pasi ambazo wanajua wenzao wanaweza kuzifikia, kila mchezaji ana aina yake ya kupigiwa pasi, mikimbio, kutafuta nafasi, hilo wachezaji wangu wengi walikuwa hawajajuana, lakini kila wanapocheza kuna kitu kipya wanakuja nacho.
Unaweza kuona sasa kila mtu ana spidi, hata wale ambao wamekuwa hawapati nafasi sasa wako fiti na utimamu wa mwili ambapo mwanzo walikuwa wanavikosa, mfululizo wa michezo umesababisha nibadilishe baadhi ya wachezaji ambapo imekuwa na faida sana kwetu, tayari nimeona tuna kikosi kipana cha wachezaji wanaoweza kucheza kama wale ambao wapo nje, hili limeonekana katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Namungo," alisema kocha huyo.
Fadlu alibainisha mpaka ikifika muda ambao unatakiwa, Simba itakuwa moto wa kuotea mbali na kuwa tayari kucheza na timu yoyote ile Afrika.