Kocha wa Manchester City Pep Guardiaola (53), huenda akaongeza mkataba wa kuendelea kuifundisha klabu hiyo, ikiwa ni baada ya miaka nane ya mafanikio na kushinda makombe sita ya Epl.
Kwa mujibu wa taarifa ya David Ornstein wa (the athletic), Guardiaola ambaye Yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake, utakaofikia tamati mwishoni mwa msimu huu huenda akaongeza mwaka mmoja zaidi, na kufanya kuondoka klabuni hapo majira ya kiangazi mwaka 2026.
Mhispania huyo, ambaye hapo awali alifundisha vilabu vya Barcelona na Bayern Munich, alifanikiwa kunyanyua Kombe la Ligi ya Mabingwa mwaka 2023, huku pia akiwa ameshinda mataji sita ya Epl katika Miaka nane tangu alipowasili klabuni hapo mwaka 2016, na kujikusanyia mataji 18 kwa jumla.
Guardiola ambaye hapo awali alitajwa kuwa huenda akachukua jukumu la kuifundisha timu ya taifa ya uingereza, kabla ya yeye mwenyewe kuzungumza kuwa anatamani kufundisha timu ya taifa siku moja, anajulikana pia kwa kutopenda kuzungumzia masuala ya mikataba yake, ambapo mkataba wake wa awali ulisainiwa Novemba 2022, ilikuwa ni takribani miezi sita kabla ya kumalizika.
Mustakabali wake umekuwa gumzo baada ya mshirika wake wa muda mrefu na mkurugenzi wa michezo wa City, Txiki Begiristain, kufichua kuwa ataondoka klabuni mwishoni mwa msimu huu.