Aliou Cisse |
Chama cha Soka Senegal kimetangaza kuachana na Kocha wa timu ya taifa, Aliou Cisse ambaye mkataba wake ulimalizika Agosti, mwaka huu.
Cisse ambaye amekuwa akiinoa Senegal tangu 2015, ni mmoja kati ya makocha waliopata mafanikio makubwa akiwa na Senegal, ikiwemo kuiwezesha kushinda taji la Afcon 2021 baada ya kuichapa Misri kwa penalti 4-3.
Vilevile aliiwezesha kushinda Kombe la CHAN 2022 katika michuano iliyofanyika 2023 nchini Algeria.
Mbali ya kushinda makombe hayo, Cisse pia aliiongoza Senegal kucheza hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2022 kwa mara ya kwanza tangu 2002.
Katika michuano ya Afcon 2019 aliifikisha timu hiyo fainali mara ya kwanza tangu 2002 ingawa ilipoteza mbele ya Algeria kwa bao 1-0.
Cisse anaachana na Senegal akiwa ndiye kocha aliyedumu muda mrefu katika nafasi hiyo kuliko yeyote kwenye historia ya taifa hilo.
Taarifa zinaeleza kwamba kwa sasa Pape Thiaw ambaye ni kocha msaidizi atachukua nafasi ya Cisse wakati mchakato wa kutafuta kocha mpya ukiendelea.
Cisse ambaye ana uraia wa Senegal na Ufaransa alianza safari ya ukocha akiwa na Louh-Cuiseaux ya Ufaransa alikodumu kama kocha msaidizi kabla ya kurudi Senegal kufundisha timu za taifa za vijana katika ngazi tofauti na baadaye kupewa mikoba ya kuinoa Senegal kuanzia Machi 2015.