Mahakama Yaifuta Kesi ya Mwijaku na Kipanya

Mahakama Yaifuta Kesi ya Mwijaku na Kipanya


Mahakama Kuu ya Tanzania (Masijala Ndogo ya Dar es Salaam) imeondoa kesi ya kashfa ya Ally Masoud Nyomwa maarufu Masoud Kipanya dhidi ya Burton Mwemba 'Mwijaku', kutokana na dosari za usajili.


Mheshimiwa Jaji David Ngunyale aliiondoa kesi hiyo mnamo tarehe 24 Oktoba 2024 kabla hajatoa uamuzi wa mapingamizi manne ya kisheria ya mdaiwa Mwijaku yaliyokwishasikilizwa kupitia Wakili wake, Gideon Opanda aliyepambana na jopo la mawakili wanne wa Kipanya wakiongozwa na Wakili Alloyce Komba.


Mahakama ilibaini yenyewe kwamba kesi iliyokuwa ikiiendesha ilisajiliwa kwa makosa kama kesi ya madai ya kawaida (normal civil suit) badala ya kuwa ni madai ya kashfa (defamation petition) kwa mujibu wa Kanuni za Sheria ya Habari za Mwaka 2019. Hivyo, kutokana na dosari hiyo Mahakama ikasitisha kuendelea na kesi ya msingi na kuiondoa.


Kabla ya uamuzi huo, Jaji Ngunyale alitoa fursa kwa mawakili wa pande zote mbili kutoa maoni yao ya kisheria kuhusu dosari hiyo na nini kifanyike kuhusu kesi hiyo ambapo Wakili wa Kipanya, Wakili Komba alisema kesi iondolewe na kumpa fursa nyingine mteja wake kufungua tena kesi hiyo ikiwa ataamua kufanya hivyo. Wakili wa Mwijaku, Wakili Opanda aliomba kesi iondolewe kwa gharama kutokana usumbufu wa kushitakiwa mteja wake.


Mahakama ilitoa amri ya kuondoa kesi yenye dosari ya usajili bila gharama ya usumbufu ikisema hoja ya dosari ya usajili iliibuliwa na Mahakama yenyewe (the issue was raised suo motu) na siyo na Wakili wa Mwijaku hivyo hapaswi kunufaika nayo.


Katika kesi ya msingi Kipanya alimshitaki Mwijaku kwa kumkashifu kupitia akaunti yake ya Instagram kwamba anafanya biashara haramu ya kuharibu vijana na kupitia katuni zake huwa anahongwa ili kuwadhalilisha viongozi wa Serikali wakiwemo Rais wa nchi. Hivyo akadai fidia ya shilingi bilioni tano na milioni mia tano (5.5bn/-) kwa madhara ya kashfa ya kushushushiwa hadhi ambayo ameijenga katika jamii kwa zaidi ya miaka thelathini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad