Mahakama Kuu nchini Kenya kwa mara ya pili imekataa kutoa amri ya kusimamisha kesi ya kumuondoa madarakani Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Suala hilo lilitajwa jana mbele ya Jaji Bahati Mwamuye, aliyeelekeza shauri lililofunguliwa na Cleopas Malalah liwasilishwe mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita kwa maelekezo zaidi.
Gachagua anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu, rushwa, kukiuka katiba, ufisadi na kudaiwa kuwa mnyanyasaji.
Kwa mujibu wa Wakili Steve Ogola, amesema kuwa huenda mahakama imetoa uamuzi huo baada ya Naibu Gachagua kuchukua uamuzi wa kuomba msamaha kwa bosi wake, Rais William Ruto, iikiwa ni sehemu ya kuthibitisha kukiri makosa.
Awali, Gachagua aliomba radhi wakati wa ibada jijini Nairobi na kusema kama kuna aliyemkosea akiwa Naibu Rais, amsamehe kutoka moyoni, alimuomba msamaha Rais Ruto, wabunge waliowasilisha hoja katika Bunge la Taifa ya kumwondoa madarakani kwa makosa aliyoyafanya.