Mahakama Yasema "Afande" Alieagiza Kubakwa Binti wa Yombo hana hatia
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imetupilia mbali maombi ya upande wa Mlalamikaji aliyewasilisha pendekezo kuwa ‘Afande’ Fatma Kigondo anayeshtakiwa kuwatuma Vijana kumbaka na kumuingilia kinyume na maumbile kwa kundi Binti Mkazi wa Yombo, asomewe mashtaka popote alipo badala ya kufika Mahakamani ikidaiwa ni mgonjwa.
Wakili Aron Kishai aliyemwakilisha Wakili Peter Madeleka amesema Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Nyamburi Tungaraja amesema maombi hayo hayajakidhi vigezo vya kisheria na kwamba haoni kosa la Mshtakiwa huku akitoa nafasi ya kukata rufaa kwa Walalamikaji kama hawajaridhika na uamuzi.
“October 16,2024 tulifika hapa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya alisema leo atatoa maamuzi ya kwamba Hakimu atoe maamuzi ya kwenda kumsomea mashtaka Afande popote alipo hata Hospitali lakini leo Hakimu ametupilia mbali maamuzi hayo akisema kifungu cha 128 hakijaonesha kosa alilolifanya Mshtakiwa”
Ikumbukwe October 16, 2024, upande wa Mlalamikaji uliwasilisha ombi hilo, ambapo Hakimu Tungaraja aliahidi kupitia sheria kabla ya kutoa maamuzi ya kusaini au kutosaini hati ya mashtaka kama ilivyoombwa.