Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali shauri lililokuwa limefunguliwa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha, Bodi ya Sukari Tanzania, Kamishna Mkuu wa TRA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na makampuni matatu ya binafsi.
Uamuzi huo umetolewa leo, Ijumaa, Oktoba 25, 2024.
Mahakama ilikubali mapingamizi yaliyowekwa na upande wa utetezi, akiwemo Jamhuri na makampuni binafsi, ambayo yalidai kuwa shauri hilo halikupaswa kuwasilishwa kama la Kikatiba.
Upande wa utetezi ulishauri kuwa Mbunge Mpina angeweza kutumia njia nyingine zaidi ya Mahakama kuwasilisha madai yake.
Mahakama ilisema kwamba pingamizi hilo pekee lilitosha kutupilia mbali shauri hilo kwa sababu ya utaratibu usio sahihi uliofuatwa.
Katika shauri lake, Mpina alikosoa utaratibu wa serikali kutoa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje na misamaha ya kodi kwa makampuni, akidai kuwa hatua hizo zimedhihirisha upotevu wa mapato ya serikali kiasi cha shilingi trilioni 1.5.
Alieleza kusikitishwa na uamuzi wa Mahakama na kuahidi kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufani, akisema anapigania maslahi ya Watanzania.
Maamuzi haya yanakuja siku moja tu baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali shauri jingine la Mpina dhidi ya Spika wa Bunge, ambapo alikosoa uamuzi wa kusimamishwa vikao vya Bunge 15.
Kwa sasa, kesi moja pekee inayohusiana na sakata la sukari inabaki Mahakamani, ambayo ni ile iliyofunguliwa na wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero.