Jumla ya Maofisa 108 wa ngazi za juu Katika ofisi ya aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua pamoja na baadhi ya washauri wakuu wa Naibu Rais huyo wamepewa agizo la kwenda likizo ya lazima.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, ilibainisha kuwa utekelezaji wa agizo hilo ulianza juzi, Jumamosi, saa 6:00 mchana, ikielezwa kuwa katika barua ya ndani ya usimamizi, mamlaka hiyo pia imesitisha mikataba yote ya wafanyakazi wa kandarasi za muda.
"Maofisa wote walioorodheshwa katika vikundi vya kazi T na U wanaagizwa kwenda likizo ya lazima mara moja," ilisoma risala iliyoandikwa na Patrick Mwangi, Katibu Mkuu Tawala katika Ofisi ya Naibu Rais.
Hayo yanajiri wakati Rais William Ruto, anakabiliwa na changamoto nyingine ya kumteua atakayeshikilia wadhifa wa Naibu Rais, huku kesi za kupinga chaguo lake zikiwasilishwa mahakamani.
Kwa upande mwingine Mahakama nchini humo iliagiza Ijumaa, kusitishwa utekelezwaji wa kumoundoa Gachagua kutoka ofisini pamoja na mchakato wa kumteua mrithi wake hadi Oktoba 24. mwaka huu, ambako kesi hiyo itaamuliwa mbele ya jopo la majaji watatu.