Serikali ya Samia Yampa Tano Paul Makonda "Piga Kazi Asikubabaishe Mtu"




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amemsihi Paul Makonda, pamoja na viongozi wengine Mkoani Arusha, kuendelea kuchapa kazi na kutojali maneno ya wapinzani mitandaoni.

Mchengerwa alitoa ujumbe huo wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 4, 2024, katika Uwanja wa Mabasi wa Kilombero.

Akizungumza mbele ya wakazi wa Arusha, Mchengerwa alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo nchini, huku akionyesha kuridhika na jitihada zinazofanyika mkoani humo.

Alibainisha kuwa kasi ya maendeleo iliyopo inatokana na kazi nzuri ya uongozi wa mkoa wa Arusha, ambao licha ya changamoto za siasa za "maji taka," umeweza kusonga mbele na kuwanyamazisha wakosoaji ambao wamebaki kuzungumza mitandaoni.


"Arusha tumejichelewesha wenyewe kwa siasa za maji taka, lakini leo hii kwa uongozi uliopo kazi inafanyika, na wale wababaishaji wamebaki kuzungumza mitandaoni tu. Paul Makonda, chapa kazi, mtu asikubabaishe," alisema Mchengerwa, akimpongeza Makonda kwa juhudi zake za maendeleo.

Mchengerwa pia aliipongeza serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo mkoani Arusha, hatua ambayo imeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo miundombinu, elimu, na afya.

Waziri alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kujitolea na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko endelevu kwa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad