Stars Ugenini Kuivaa Sudan Kusaka Tiketi Fainali CHAN



 Stars Ugenini Kuivaa Sudan Kusaka Tiketi Fainali CHAN

KIKOSI cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, leo saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kitajitupa kwenye Uwanja wa de la Capitale, jijini Nouakchott, nchini Mauritania kucheza mechi ya mtoano, kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za mataifa kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), huku Kocha Mkuu, Bakari Shime akisema wapo tayari kwa mapambano.


Stars, inayoundwa na wachezaji wanaocheza hapa nchini, ipo chini ya kocha Shime, inacheza mechi hiyo nchini humo badala ya Sudan kutokana na nchi hiyo kuwa na machafuko ya vita kwa wenyewe kwa wenyewe.


Kocha Shime amesema kila kitu ambacho kinahitajika kwa ajili ya mchezo huo, kimefanyika na kinachosubiriwa ni wachezaji wake kuingia uwanjani, ili wakalipambanie taifa.


"Nawaamini vijana wangu, kuna watu wanasema wengi hawana uzoefu, ni kweli, lakini hawana uzoefu kwenye michezo ya kimataifa tu, lakini wana uzoefu wa kucheza kwenye klabu zao za Ligi Kuu, naamini wanaweza kwani hata wale ambao ni wazoefu walianza kama hawa," alisema Shime.



Kati ya wachezaji 24 walioteuliwa kuunda kikosi hicho, 11 wanatoka timu ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes iliyotwaa Ubingwa wa CECAFA hivi majuzi nchini, kwa kuifunga Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.


Kuhusu kipa Aishi Manula, alisema yeye atakuwa kama kocha wa ndani na ndiyo maana amemchukua kwenye kikosi hicho.


"Kwangu mimi kumchagua Manula nilichohitaji ni mdomo wake zaidi kuliko mikono yake,"


Hoja ni kwamba hajacheza muda mrefu, lakini Aishi yupo sawasawa, nafasi anayocheza ni ya golikipa na kama unavyoona wachezaji wote kwenye timu yetu wanaocheza nafasi ya ulinzi ni chipukizi, kwa hiyo wanamhitaji mtu nyuma yao ambaye anaweza kufanya kazi kama yangu mimi niliye kwenye benchi, namna gani anaweza kupeleka maelekezo sahihi na kuwafanya mabeki na wachezaji wote kucheza katika utaratibu unaotakiwa," alisema.


Baada ya mechi hiyo, timu hizo zitacheza mchezo wa marudiano, Novemba 3, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Fainali za CHAN zinatarajiwa kufanyika hapa nchini, Uganda na Kenya, kuanzia Februari Mosi hadi 28 mwakani.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad