TCRA YASIMAMISHA LESENI YA MWANANCHI KURUSHA MAUDHUI MTANDAONI

TCRA YASIMAMISHA LESENI YA MWANANCHI KURUSHA MAUDHUI MTANDAONI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mtandaoni (online media services licences) za kampuni ya Mwananchi Communications Limited, wachapishaji wa magazeti na mitandao ya The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti.

Taarifa iliyotolewa na TCRA kwa umma leo Oktoba 2, 2024 imesema leseni za kutoa huduma za maudhui mtandaoni zimesitishwa kwa muda wa siku 30 kuanzia leo wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi.

Taarifa imeonesha kwamba jana Oktoba 1, 2024 Mwananchi Communications Limited ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual content) kwenye mitandao yake ya kijamii, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni.

“Aidha, maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa Taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandao (the Online Content Regulations) za mwaka 2020, Mwananchi Communications Limited na wengine wote wenye leseni, wanatakiwa kutokutangaza au kuchapisha kwa umma maudhui yaliyozuiwa ikiwa ni pamoja na maudhui yanayolenga kudhihaki au kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

TCRA ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania, Sheria Na. 12 ya mwaka 2003, kusimamia huduma za mawasiliano ya Kielektroniki na Posta katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad