Wakili Edwin Mugambila, amesema sababu ya mtuhumiwa anayetajwa kwa jina la ‘afande’, kutounganishwa katika kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Saalam, kunatokana na ushahidi duni na kukosa muunganiko wa picha na afande.
Amesema licha ya umma hususan kwenye mitandao ya kijamii kupaza sauti kudai mtu anayetajwa kuwa ni afande alihusika kuwatuma vijana hao wanne waliokutwa na hatia mwishoni mwa wiki, ushahidi ulikosa muunganiko kati ya anayetajwa na picha aliyooneshwa binti, ili athibitishe.
Wakili huyo akizungumza jana, kupitia redio ya Clouds Fm, jijini Dar es Salaam, alisema kesi hiyo ilibeba hisia kali kijamii kulikuwa na maombi takribani 20 yaliyowasilishwa mahakamani, huku makundi ya mawakili zaidi ya matatu yakiomba kuifuatilia, huku ikiendeshwa kwa takribani miezi miwili hadi hukumu, akisema, lengo ni kumpunguzia msongo mtendewa.
“Binti (binti wa Yombo) mwenyewe tulipomhoji alisema picha aliyoonyeshwa kwamba ndiye afande alikuwa jinsi ya kiume, mijadala ilikuwa ni mingi na hisia zilikuwa nyingi. Hata sisi (mawakili) ilituletea confusion (mkanganyiko) sana.
Binti, wakati wa tendo likiendelea alikuwa anaambiwa ‘muombe msamaha huyu…’ mimi sikuiona hiyo picha, ila kinachoelezwa na wahusika wakati wa kuchambua ushahidi, washtakiwa wenyewe Nyundo na wenzake, walisema ilikuwa picha ya mmoja wetu (washtakiwa).
Lakini sasa pamoja na hiyo ’confusion’ mnafanyaje, mnahitaji japo chembe ya kum-konekti huyu mtu (afande) na tukio? IIi kupambana huyu mtu aletwe mahakamani kama mshtakiwa. Kulikuwa hamna muunganiko,” alisema wakili huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu.
Kinachoelezwa ni kwamba walichukuana baa (binti na washtakiwa) kwa maandalizi fulani fulani, wameanza kumfanyia kile kitendo wakimwonesha picha, huku wakimtaka aombe msamaha kwa picha ya mwanamume, haijulikani alikuwa ni nani ila ni miongoni mwao.
Sasa ili yule mama (anayetajwa kuwa afande), aingie katika mashtaka ni lazima mmoja wa wale vijana wamtaje au shahidi yeyote, tofauti na hapo atatajwa yeyote kama hakuna ushahidi, hakuna muunganiko wa tukio hata sisi wenyewe tulitaka apelekwe mahakamani, lakini ushahidi uko wapi, labda kitakachofanyika ni ushahidi wa kimazingira.”
Alisema kuhusu adhabu zilizotolewa dhidi ya washtakiwa hao, mbali na kifungo cha maisha jela, Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Kifungu cha 348, kinatoa mwongozo kwa makosa ya kijinsia ‘sexual offences’ ni lazima mwathirika kupewa fidia.
“Kiasi gani cha fidia anatakiwa apewe, hilo ni kwa jaji au hakimu, ndio maana akatoa amri wale vijana wote watoe shilingi milioni moja kila mmoja. Ingawa kuna madhara amepata huyo binti, madhara iliyopata familia wanaweza kufungua shauri la madai, kwa madhila aliyopitia, msongo na muda aliopoteza na mahangaiko kifamilia,” alisema wakili huyo.
“Inategemeana na wanaweza kuomba fidia ya kiwango chochote hata Sh. bilioni 200 kutokana na tathmini ya mahakama ya madhara aliyoyapata, itakavyoona inafaa. Na kama wana mali waliohukumiwa…au kwa nchi zilizoendelea kuna mfuko maalum wa fidia kwa waathirika wa matukio kama hayo.
Au njia ya pili kama waliohukumiwa wana mali, zile mali zinakamatwa na kuuzwa kulipia fidia. Kwa uzoefu tulionao ni nadra hili kutokea, ila kwa kuwa anasimamiwa na taasisi za kisheria, tuna imani wanaweza kusimamia hilo.”
Washtakiwa wanne katika kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Saalam, mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, hivi karibuni.
Washtakiwa hao walikuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo na Amin Lema, maarufu Kindamba.
Wengine ni Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi pamoja na Nickson Jackson, maarufu Machuche.
Agosti 19, mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kunyume cha maumbile binti huyo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, iwapo wakithibitika kutenda ukatili huo, watakumbana na adhabu ya kifungo cha maisha gerezani