Anayeshtakiwa Kumuua Mkewe na Kumchoma Kwa Magunia ya Mkaa Akutwa na Kesi ya Kujibu

Anayeshtakiwa Kumuua Mkewe na Kumchoma Kwa Magunia ya Mkaa Akutwa na Kesi ya Kujibu


MFANYABIASHARA Khamis Luwongo (38) anayeshtakiwa kwa kumuua mkewe Naomi Marijani kisha kuuchoma moto mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, amepatikana na kesi ya kujibu, baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi 14 wa upande wa mashtaka.


Aidha, wakili wa mshtakiwa, Hilda Mushi, aliiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imruhusu mteja wake atumie ripoti iliyotoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe iliyoonesha kwamba wakati akitenda kitendo hicho, hakuwa timamu. 


Jaji Hamidu Mwanga  alitoa uamuzi huo juzi baada kupitia ushahidi uliotolewa na pamoja na vielelezo na kuona mshtakiwa ana kesi ya kujibu na atatakiwa kujitetea. Baada ya kuelezwa ana kesi ya kujibu, mshtakiwa alidai atajitetea kwa kiapo. 


Mahakama pia ilipokea vielelezo mbalimbali katika kesi hiyo kama nyaraka ya maelezo ya onyo, maelezo ya ungamo, simu, laini za simu na udongo wenye masalia ya mafuta yanayodhaniwa kuwa ni ya Naomi.


 Licha ya kuomba kutumia taarifa ya afya, mbele ya Jaji Elizabeth Mkwizu, mshtakiwa alikataa kwenda kupimwa akili na kudai kwamba yeye ni mzima wa afya na hana tatizo la akili, hivyo kwenda Mirembe ni kupoteza muda.



 Pia akiwa mbele ya Jaji Mwanga, alidai  kwamba aliyekuwa wakili wake, Mohamed Majaliwa, alishindwa kumzuia kwenda kupimwa akili Mirembe kwa madai kuwa  yuko timamu.


 Jaji Mwanga alikubaliana na ombi hilo la mshtakiwa kutumia ripoti hiyo katika utetezi wake ambayo iko kwenye mwenendo wa kesi hiyo.


Wakati Shahidi wa 13, Koplo Samwel, anatoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter, alidai kuwa mwaka 2019 alikuwa akifanya kazi Kituo cha Polisi Kigamboni.


Alidai kuwa Julai 16, 2019 saa 8:00 mchana, akiwa kazini alielekezwa na Mkuu wa Upelelezi, Malelo kuongoza na timu ya upelelezi kwenda Gezaulole kwenye nyumba ya Khamis au Meshack ili kufanya upelelezi, akiwaongoza na mshtakiwa mwenyewe.


 "Kiongozi wa msafara aliwaita  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Mjumbe na Khamis aliwaongoza ndani ya nyumba yake akawaonesha sehemu alikomuulia marehemu,"alidai Koplo Samwel


 Alidai kuwa mshtakiwa Khamis aliwaonesha sehemu marehemu alikodondokea na kulikuwa na damu chini na kitandani na wataalamu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi waliendelea na kazi yao.



 Pia aliwaongoza alikotoa nje mwili wa marehemu kwenye banda la kuku ambalo alitengeneza shimo akaujaza mkaa akauchoma na akawaonesha sehemu ambayo alimchomea moto.


 Alidai kuwa kwenye banda hilo kulikuwa na damu ambayo mshtakiwa alidai ni zake ambazo alijiumiza wakati akitoa masalia ya marehemu ambayo aliyatia kwenye mfuko wa saruji na kuyapeleka kijiji cha Marogoro,  Mkuranga mkoani Pwani.


"Nilichora ramani ya tukio mahali mauaji yalifanyika na mwili ulikochomewa.


Kisha mshtakiwa aliwaongoza katika Kijiji cha Marogoro Kata ya Vikindu Wiliaya ya Mkuranga,"alidai Koplo Samwel


Koplo Samwel alida walipofika eneo hilo kiongozi wa msafara aliwaita majirani pamoja na viongozi wa kijiji na mshtakiwa aliwapeleka sehemu alikozika masali ya mwili wa marehemu ambako wakikuta mashina matatu ya migomba.


 Alidai kuwa mshtakiwa aliwaeleza kuwa mabaki ya mwili wa marehemu aliyazikia kwenye mgomba wa kwanza,walifukua kwenye wakakuta masalia majivu na mafuta na mifupa na meno yaliyoungua.


 "Timu ya ‘forensic’ iliendelea na kazi yao yeye alichora ramani ya eneo la tukio akiongozwa na mshtakiwa Luwongo. Wakati anatuongoza alikuwa kwenye hali nzuri na ndio maana tulipofikia shambani alituonesha kuwa masalia ya marehemu aliyazima kwanya mgomba huu," alidai.


 Alidai kuwa walifika shambani jioni saa 12:30 jua likiwa limeshazama, hivyo walitumia mwanga wa tochi na taa za magari waliyokuwa nayo. Luwongo alitia saini ramani hizo zote, kazi hiyo ilimalizika saa 4:00 usiku.


 Pia shahidi wa 14, Koplo Mkombozi, ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Polisi  akiongonzwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, alidai kuwa mwaka 2019 alikuwa anafanya kazi Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Ofisi ya ZCO (Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam)


Alidai kuwa alielekezwa na kiongozi wake akaandae timu ya ukaguzi wa matukio na mtuhumiwa aliwaongoza kuwapeleka eneo la tukio.

By Grace Gurisha , Nipashe

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad