BAADA ya kutambulishwa rasmi na Zesco United, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Freddy Michael Koublan, amejipanga kurejea kwa kishindo kwenye soka la ushindani.
Mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast, anarejea kwenye Ligi Kuu ya Zambia baada ya kupita takribani miezi 11 tangu aondoke Green Eagles Januari 2024 na kutua Simba.
Freddy aliyeitumikia Simba kwa kipindi cha miezi sita akifunga mabao manane katika mechi 13, amejiunga na Zesco United kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kukaa kwa muda bila ya timu.
“Nilifurahia maisha yangu ya soka Tanzania na nilikuwa na nafasi ya kuendelea kucheza huko kutokana na timu ambazo zilivutiwa na mimi lakini nashukuru Zesco kwa imani kubwa zaidi waliyoonyesha juu yangu,” alisema mshambuliaji huyo.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Zesco United, ilisema: “Zesco United Football Club ina furaha kutangaza usajili wa mshambuliaji wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Freddy Michael Koublan, kwa mkataba wa mwaka mmoja.”
Freddy wakati anatua Simba dirisha dogo msimu uliopita 2023-24, aliondoka katika Ligi Kuu ya Zambia akiwa na mabao 14 yaliyomfanya kuongoza orodha ya wafungaji kunako ligi hiyo.
Akizungumzia malengo yake akiwa na Zesco United, Freddy alisema: “Nina kazi kubwa ya kufanya, na naamini tutafikia mambo makubwa msimu huu. Kama mnavyonijua, mimi ni mtu wa malengo na nipo hapa kutoa mchango wangu.”
Kocha wa Zesco United, George Lwandamina, alizungumza kuhusu usajili wa Freddy kwa kusema: “Freddy ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na historia nzuri ya kufunga mabao. Tunamuhitaji sana katika safu yetu ya ushambuliaji, na tunaamini atatusaidia kutimiza malengo yetu.”