Gamondi ni mtu wa kula bata. Wakati mwingine anaungana na wachezaji wake kula maisha. Na unapokuwa kocha wa Yanga au mchezaji wa Yanga, maisha yanakuwa matamu zaidi. Papo hapo kushika mambo mawili kwa wakati mmoja inakuwa shida.
.
Yanga ya msimu huu sio ya msimu uliopita. Aziz Ki anapoteza mipira ovyo. Ameridhika. Pacome Zouzoua naye ameridhika. Anacheza kawaida tu na wala hawaachi midomo wazi mashabiki kama ilivyokuwa msimu uliopita. Katika mechi ngumu lazima wapangwe na Clatous Chama akae katika benchi. Kisa? Gamondi amekariri na anataka kuendesha maisha rahisi kwa wachezaji wake.
.
Wakati Aziz akipoteza mipira ndani, Chama anakuwa ameshika tama katika benchi. Gamondi anaamini kwamba kuna jambo tu litatokea. Matokeo yake zile tano tano za msimu uliopita zimetoweka. Kwa namna walivyokuwa wanacheza siku moja niliwahi kukaririwa nikizungumza redioni Wasafi kwamba Yanga alikuwa wanakaribia kufungwa au kutoka sare.
.
Na kweli. Pambano dhidi ya Tabora hatimaye limevunja mzizi wa fitina. Limewaamsha rasmi Yanga kwamba wanapokwenda sio njia sahihi. Kuna wanaosema atafukuzwa muda mfupi ujao. Kuna wanaosema anaweza kuendelea kuwepo. Hata hivyo suala la kuwepo kwa uvumi tu ni dalili tosha kwamba fungate ya Gamondi na imefika mwisho.
.
Timu zetu hazijawahi kuwa na uvumilivu ambao Gamondi anadhani tunao. Timu zetu pia haziangalii sana historia wala rekodi zako katika msimu uliopita. Zinaishi kwa ajili ya sasa.
.
Yanga hii ambayo Aziz Ki anapoteza mipira anacheka huku akimtazama mrembo wake jukwaani inaweza ikamfanya Gamondi asifike Krismasi. Anahitaji kuwafanya wachezaji wasiwe katika ‘comfort zone’ kama ambavyo wamekuwa msimu huu. Ni mlokole Maxi Nzengeli tu ndiye ambaye anaonekana kuwa na hamu na mpira. Wengine wanacheza huku wakiwa wametanua makwapa.
.
Bahati mbaya ambayo Gamondi anaweza kupita kwa sasa na mwenyewe haijui ni kwamba kuelekea katika uvumi wa kufukuzwa hakuna mashabiki au wanachama ambao watajitokeza na kumkingia kifua. Hii ni kwa sababu wanachama na mashabiki wanaamini zaidi katika uamuzi wa rais wao kijana, HERSI SAID na kamati yake ya utendaji.”