Benard Morrison Aitolea Nyongo Ghana Baada ya Kushindwa Kufuzu AFCON, Walinibagua



Benard Morrison Aitolea Nyongo Ghana Baada ya Kushindwa Kufuzu AFCON, Walinibagua

Winga Bernard Morrison ameishutumu timu ya taifa ya Ghana kwa kuwa na ubaguzi katika kuita wachezaji wa timu ya taifa jambo analoamini linachangia ifanye vibaya katika mashindano mbalimbali.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na Simba, ametoa lawama hizo muda mfupi baada ya Ghana kushindwa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco, baada ya kushika mkia katika kundi F la mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo nyuma ya Angola, Sudan na Niger.

Kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kutoka kwa Niger kiliifanya Ghana imalize mashindano hayo ya kufuzu ikiwa haijapata ushindi hata mara moja, ikitoka sare tatu na kupoteza tatu na Morrison anaamini kuwa kuna wachezaji wengi hawastahili kuchezea timu hiyo ya taifa.

"NCHI INAYOITWA GHANA. Heshima ya kutosha kwa Niger lakini Ghana haiwezi kuifunga hii timu ya Niger? Nilikuwa shabiki mkubwa wa timu yetu ya taifa kipindi hicho hadi 2017 hadi sasa. Niliacha kuiangalia Ghana kuanzia 2018 kwa sababu nilipojiridhisha kuwa hakuna nafasi kwangu.

"Nimecheza AS Vita Club ya DR Congo, Orlando Pirates Afrika Kusini, Yanga na Simba za Tanzania. Tumecheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika ambazo nimekuwa sehemu muhimu kwenye klabu hizo lakini sitambuliki kwa sababu nacheza Afrika.

"Lakini wanaita wachezaji kutoka daraja la pili na daraja la tatu Ulaya kuwakilisha Ghana. Wanaita wachezaji wa ligi ya Ghana ambao klabu zao haziwezi hata kupata ushindi kwenye mechi za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati mwingine hadi wachezaji ambao klabu zao zinashika mkia kwenye msimamo wa ligi wanaitwa," alisema Morrison.

Morrison alisema kuwa anaamini wachezaji wengi wazuri hawaitwi kwa sababu hawana watu wa kuwapigia kampeni ndani ya Chama cha Soka Ghana.

"Lakini sisi tunaoiwakilisha nchi nje katika klabu kubwa na kushinda mataji ya ligi hatuonekani kwa sababu hauna mtu yeyote katika shirikisho wa kukupigania. Kuna wakati wachezaji wanaitwa wakiwa hawapati hata nafasi ya kuanza katika ligi daraja la tatu Ulaya. Inafurahisha.


"Kila mmoja atakuwa na furaha kuona mwanafamilia wake yupo katika rangi za taifa ndio lakini sidhani kama hawa wachezaji kuanzia 2018 hadi sasa ni bora kunizidi. Sio mbinafsi na sijiamini lakini ni ukweli. Nisingepata ujasiri wa kuizungumzia uteuzi wa timu ya taifa kabla ya 2017. UBORA. Haya mataifa tunayoshindwa kuyafunga yana wachezaji ambao tunakutana nao na tunawapita tukiwa na mpira wakati wa mechi za ligi na Ligi ya Mabingwa lakini unatuona sisi hatuna ubora wa kutosha kuichezea Ghana. Ni ujinga," alisema Morrison.

Mchezaji huyo aliongeza kwamba kuna urasimu mkubwa unaofanywa na Chama cha Soka Ghana katika uteuzi wa wachezaji wa timu yao ya taifa.

"Hakuna klabu ya Ghana ambayo inaendana na nishati na daraja la ubora la klabu ambazo nimechezea lakini wachezaji walio katika timu zilizo katika mstari wa kushuka daraja wanaitwa. Chama cha familia ya soka Ghana, hakuna uadilifu, uwazi na usawa halafu unataka matokeo?.


"Hizi Niger, Sudan, Angola, DR Congo, na nyinginezo vikosi vyao vingi vina wachezaji wa ligi za Afrika na wanaziwakilisha vizuri nchi zao lakini unafikiria wanaocheza Ulaya ni bora kutuzidi. Ni vile tu baadhi yetu hatujapata mawakala wa kutuunganisha Ulaya.

"Hawa washambuliaji na mawinga wa Black Stars ni bora kuliko sisi? Kuanzia 2017 nimekuwa na lengo la kulisha familia yangu," alisema Morrison.

Mara ya mwisho kwa Ghana kuchukua ubingwa wa Afcon ilikuwa ni 1982 na baada ya hapo, mafanikio makubwa kwa timu hiyo kwenye mashindano hayo ilikuwa ni 2008 iliposhika nafasi ya pili.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad