STAA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Harmonize amepiga marufuku wimbo wake maarufu wa 'Yanga Bingwa' kuchezwa sehemu yoyote hadi pale atakapotoa taarifa nyingine kuhusu wimbo huo.
Harmonize ametoa maelekezo hayo kupitia mtandao wa Instagram, ikiwa ni saa chache tangu Yanga ifumuliwe mabao 3-1 na Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
"Sitaki wimbo wangu wa YANGA BINGWA upigwe sehemu yeyote sio kumbi za sterehe wala sehemu yoyote yenye mkusanyiko hadi nitakapowajulisha. Asanteni sana." Ameandika Harmonize maarufu kama Konde Boy.
Mbali na taarifa hiyo, Harmonize ameshangazwa na kitendo cha mwimbaji mwenzake, Tunda Man ambaye ni shabiki wa Simba kufanya sampling ya wimbo huo bila kupata kibali kutoka kwake.
"Nikimfikisha mahakamani namuonea?? Sina shida na hela ila inani disturb, Makolo wautumie huo wimbo kwenye kipindi matokeo haya mapya na mabaya kwetu!! Nakuheshimu Tunda futa huo wimbo." alisisitiza staa huyo ambaye ni Yanga lialia na wimbo huo wa Yangaa Bingwa wenye kibwagizo cha Yanga hii unaifungaje, imekuwa ikitumiwa na mashabiki wa Simba kuwajeli watani wao tangu timu hiyo ilipolazwa 1-0 na Azam kabla ya jana usiku kufumuliwa 3-1 na Tabora mechi zote watetezi hao wao wenyeji wa mchezo.