Hesabu Tamu Zinaibeba Tena Yanga Ligi Kuu Bara

 


Licha ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam FC wikiendi iliyopita, lakini hesabu za Yanga bado ni tamu kulinganisha na washindani wake wakubwa ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu.


Yanga ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara ikibeba taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo, msimu huu mpaka sasa inaonekana washindani wake wakubwa ni Simba, Azam na Singida Black Stars.


Hiyo inatokana na namna timu hizo zilivyojikatia kipande chao kwenye nafasi nne za juu za msimu wa ligi hiyo iliyobakisha mechi chache kumaliza mzunguko wa kwanza.


Kitendo cha Yanga kufungwa na Azam, kimeifanya timu hiyo kupunguzwa kasi tu lakini bado imeendelea kukaa kileleni licha ya kuwa na michezo pungufu ukilinganisha na wanaomfuatia kwa ukaribu, Azam na Singida Black Stars zilizocheza 10 kila mmoja, huku Simba ikicheza tisa kama Yanga.


Msimamo wa ligi hiyo katika nafasi nne za juu unaonyesha kwamba, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 24 ikifuatiwa na Singida Black Stars yenye 23, Simba inazo 22 huku Azam ikikusanya pointi 21.


Kesho Jumatano, Simba itaikaribisha KMC kwenye mchezo wao wa kumi huku Yanga ikicheza Alhamisi nyumbani dhidi ya Tabora United na baada ya mechi hizo ligi itasimama kwa takribani wiki mbili kupisha mechi za kimataifa.


Faida kwa Yanga


Wakati ligi ikirejea Novemba 21 mwaka huu, Yanga itakuwa na faida kubwa kuelekea kuumaliza mzunguko wa kwanza kutokana na kwamba tayari imemalizana na washindani wake wa karibu na bado inaongoza ligi.


Yanga tayari imecheza dhidi ya Simba na kushinda 1-0, ushindi kama huo imeupata mbele ya Singida Black Stars kabla ya kupokea kipigo kama hicho kutoka kwa Azam.


Katika pointi tisa ambazo Yanga ilizisaka mbele ya Simba, Singida Black Stars na Azam, imeambulia sita na kupoteza tatu.


Yanga imebakiwa na mechi sita kukamilisha mzunguko wa kwanza, kati ya hizo nne zitakuwa nyumbani dhidi ya Tabora United, Fountain Gate, Mashujaa na Tanzania Prisons, wakati za ugenini ni mbili dhidi ya Namungo na Dodoma Jiji.


Singida Black Stars katika mechi tano zilizobaki kumaliza mzunguko wa kwanza, tatu itacheza ugenini dhidi ya Tabora United, Azam na Tanzania Prisons huku mbili za nyumbani ni dhidi ya Simba na Dodoma Jiji.


Ukiangalia Singida Black Stars, bado haijamalizana na Simba na Azam, huku pia ikiwa tayari imepoteza mbele ya Yanga. Ili kubaki sehemu salama, inatakiwa kuzifunga timu hizo ili kutokuwa mbali na Yanga ambayo yenyewe imepoteza mechi moja kati ya tatu dhidi ya washindani wake.


Azam nayo imebakiwa na mechi tano, kati ya hizo nyumbani tatu dhidi ya Kagera Sugar, Singida Black Stars na Fountain Gate. Mbili ni ugenini dhidi ya Dodoma Jiji na Tabora United.


Kwa upande wa Azam, tayari imemalizana na Simba ambapo ilipoteza kwa mabao 2-0, kisha ikaifunga Yanga 1-0, bado ina kibarua cha kukabiliana na Singida Black Stars.


Simba nayo mechi sita zilizobaki kabla ya kuumaliza mzunguko wa kwanza ni dhidi ya KMC (nyumbani), Pamba Jiji (ugenini), Singida Black Stars (ugenini), KenGold (ugenini), Kagera Sugar (ugenini) na JKT Tanzania (nyumbani).


Katika mechi tatu dhidi ya washindani wake, Simba imeifunga Azam 2-0, ikafungwa na Yanga 1-0, bado haijacheza na Singida Black Stars, huku mechi zake sita za mzunguko wa kwanza zilizobaki ni nyumbani mbili na ugenini nne.


Msimu uliopita ilikuwaje?


Timu hizo nne za juu kwa sasa, msimu uliopita katika mzunguko wa kwanza Yanga ilimaliza ikiwa juu kwa kukusanya pointi 40 kati ya 45 zinazotokana na michezo 15.


Yanga katika mechi hizo 15, ilishinda 13, sare moja na kupoteza moja.


Simba ilifuatia kwa kukusanya pointi 36 ikiachwa nne na Yanga. Katika mechi 15, Simba ilishinda 11, sare tatu na kupoteza moja.


Azam katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza msimu ulioputa, ilikusanya pointi 35 zilizotokana na kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza mbili.


Singida Black Stars ambayo ilikuwa ikitambulika kwa jina la Ihefu, msimu huu imefanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake ambapo ukilinganisha na msimu uliopita, utaona kuna utofauti mkubwa sana.


Msimu huu timu hiyo ambayo sasa inashika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 10 na kukusanya pointi 23, msimu uliopita wakati ikiitwa Ihefu ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 16 baada ya kushinda mechi nne, sare nne na kupoteza saba.


Msikie Gamondi


Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema timu yake bado ipo kwenye ubora wa hali ya juu na inapambana kutetea taji la Ligi Kuu Bara.


Gamondi ambaye msimu huu ana kazi ya kutetea taji la Ligi Kuu Bara aliloshinda msimu uliopita alipoanza kazi ya kuinoa Yanga, ameliambia Mwanaspoti kwamba anafurahia nyota wake kuendelea kuwa na uhitaji wa kufanya vizuri zaidi jambo linalompa imani ya kubeba tena ubingwa.


"Najivunia kikosi changu kina wachezaji wenye uchu wa mafanikio, tumeumia pamoja kupoteza dhidi ya Azam lakini bado wananipa imani kuwa hawajakata tamaa na wanahitaji kuwa bora zaidi, hii inanipa picha ya namna gani nakuwa sina wakati mgumu kuwaongoza kwa sababu wao pia wanatamani kuwa bora," alisema na kuongeza:


"Nimekuwa na wakati mzuri na timu hii, wachezaji wangu wana morali nzuri na kila mchezaji anapambana kuhakikisha timu inafikia malengo ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kikosini kulingana na ratiba na michezo."


Gamondi alisema yeye ni muumini wa mchezo wa kushambulia zaidi na ataendelea na mfumo huo huku akikiri kuwa Yanga imara inazidi kujengwa licha ya kupoteza mchezo uliopita.


"Siwezi kubadili muundo wa uchezaji wa timu yangu hata kama tukiwa pungufu uwanjani, naamini katika ushambuliaji, hivyo kazi hiyo itaendelea kufanyika kama kawaida kutokana na aina ya kikosi nilichonacho.


"Nimekuwa nikikutana na changamoto ya timu nyingi pinzani kucheza kwa kujilinda muda mwingi, mifumo yao imekuwa ikinitesa sana na kuipa wakati mgumu timu yangu kushinda, hili nalishughulikia," alisema Gamondi.


Kwa upande wa kiungo mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho alisisitiza kuwa matokeo yaliyopita yatawarudisha wakiwa imara zaidi kuelekea michezo ijayo.


"Tumekubali tulipoteza lakini matokeo hayo sio mwisho wa mapambano yetu, tutaendelea kupambana kwa lengo la kuhakikisha tunafikia malengo," alisema Aucho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad