MABADILIKO katika benchi la ufundi la Yanga, yameonekana ‘kumtisha’, Kocha Mkuu wa Al Hilal Omdurman ya Sudan, Florent Ibenge, ambaye amesema yeye alijiandaa kupambana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi na si Mjerumani, Sead Ramovic
Yanga ilitangaza kuchana na Gamondi wiki iliyopita na Ramovic kutoka TS Galaxy ya Afrika Kusini alikabidhiwa mikoba ya kuwaongoza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa hatua ya makundi wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ibenge, alisema maandalizi waliyokuwa wameyafanya awali ni kwa ajili ya kukabiliana na mfumo unaoongozwa na Gamondi.
Ibenge alisema kwa nyakati mbalimbali alikuwa ‘ameshamsoma’ na kujua mbinu za Gamondi na kukiandaa kikosi chake kukabiliana na ushindani huo, lakini ujio na Ramovic, umemchanganya.
“Tulishamjua aina yake ya uchezaji na mifumo ya Gamondi, tulifanyia kazi namna timu yake inavyocheza, huyu mpya kwetu itakuwa ni mgumu sana, hatujui lolote, hatujui atakuja na mbinu gani. Tunatakiwa kuwa makini sana,” alisema Ibenge.
Mkongomani huyo alisema kundi lao lenye timu za Yanga, Al Hilal, MC Alger ya Algeria na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), ni gumu na kila timu ina uwezo wa kuifunga timu nyingine na kutinga hatua ya robo fainali.
“Kila timu inataka kwenda robo fainali na kundi letu (Kundi A), timu yeyote inaweza kumfunga mpinzani, zina uzani na ubora unaolingana, hivyo tunatakiwa tupate pointi nyingi kwa kadri inavyowezekana,” alisema Ibenge.
Aliongeza kwa sababu hiyo aliamua kuwasili nchini mapema kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mchezo huo ambayo ni pamoja na kuzoea hali ya hewa ya Dar es Salaam ambalo kwa sasa joto.
“Ni mechi kubwa sana kwetu, tunatakiwa kujitayarisha vizuri na umakini zaidi na ndiyo maana tumekuja mapema, unajua tunakwenda kucheza na timu kubwa sana kwa sasa Afrika, hivyo itakuwa ngumu sana kwetu, inatakiwa kuandaa mikakati ya kumsoma angalau kwa uchache kocha mpya,” aliongeza kocha huyo.
Mechi ya Yanga dhidi ya Al Hihal itachezwa Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Ramovic.
Mjerumani hiyo anakabiliwa na kibarua cha kuendeleza mafanikio yaliyoachwa na Gamondi ambaye licha ya kuiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi msimu huu baada ya mara ya mwisho vigogo hao kucheza hatua hiyo ilikuwa ni mwaka 1998.
Kikosi cha Gamondi kilitolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa penalti 3-2, mechi iliyochezwa Aprili 5, mwaka huu baada ya kutoka suluhu michezo yote miwili, mechi ya kwanza ikifanyika Machi 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.