Mabao Manne ya Musonda Timu yake ya Taifa Yawatafakarisha Viongozi wa Yanga



MABAO manne ambayo Kennedy Musonda ameyafunga katika mechi za kuwania kufuzu Mainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, yakiwemo mawili kwenye mechi mbili mfululizo za mwisho, zimewafanya mabosi wa Yanga kurudi mezani na kubadilisha mpango waliouandaa kwa ajili ya dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15, 2024 hadi Januari 15 mwakani.

Yanga ilipanga kumuacha mshambuliaji huyo ili kupisha ujio wa nyota wa Uganda, Fahad Bayo lakini baada ya Musonda kuwasha moto akiwa na kikosi cha Zambia, uongozi wa timu hiyo umeamua kumpa fursa kocha Sead Ramovic kuamua mshambuliaji gani wa kigeni kati ya Musonda, Jean Baleke na Prince Dube afungashishwe virago.

Musonda ambaye mabao hayo manne yamemfanya kuwa kinara wa ufungaji katika timu yake ya Zambia iliyofunga mabao saba katika mechi sita, ameshika nafasi ya tatu kwa ufungaji wa jumla sambamba na Amine Gouiri (Algeria / Rennes ya Ufaransa) na mshambuliaji wa Misri, Mahmoud Ahmed Ibrahim maarufu kwa jina la Trezeguet.

Kinara ni nyota wa Real Madrid na Morocco, Brahim Diaz aliyefunga saba akifuatiwa na Serhou Guirassy wa Guinea mwenye sita akiitumikia Borussia Dortmund.

Kwa maana hiyo, Dube, Musonda na Baleke kila mmoja anapaswa kuzitumia vyema mechi nne zilizo mbele yao kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa ili kila mmoja kupigania hatima yake klabuni hapo, ingawa presha hiyo haimgusi Clement Mzize.

Kabla ya kufunguliwa kwa usajili wa dirisha dogo, Yanga itacheza mechi nne zikiwemo tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal (Novemba 26), MC Alger (Desemba 7) na TP Mazembe (Desemba 14). Pia mechi moja ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo (Novemba 30).

Mmoja wa vigogo wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa mpango wa kumuacha Musonda umefutwa na yeyote kati yake, Dube au Baleke anaweza kuondoka ikiwa kocha Ramovic hatoridhishwa na kiwango chake kipindi hiki kabla ya dirisha dogo la usajili.

“Musonda ilikuwa aachwe dirisha dogo lakini ukiangalia kile anachokifanya akiwa na timu ya taifa ya Zambia inafikirisha kiukweli na tukahisi huenda tatizo likawa ni kocha aliyepita (Miguel Gamondi) alishindwa kumtumia vizuri hivyo sasa yeye na mwenzake (Baleke) kila mmoja anapaswa kujipigania katika mechi zilizopo kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa ili kushawishi timu imbakishe.

“Mwanzoni ilikuwa yeye ndio aondoke lakini usije kushangaa kuona akiachwa Baleke ikiwa Musonda atahamisha makali ya kile anachokifanya Zambia ndani ya Yanga,” kilifichua chanzo hicho.

Takwimu za Musonda msimu huu Ligi Kuu Bara zinaonyesha, amecheza dakika 142 katika mechi saba kati ya 10 ambazo Yanga imecheza, akifunga bao moja.

Msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara alicheza mechi 22 kwa dakika 1116, akifunga mabao matano, asisti mbili, huku akipiga mipira iliyolenga goli 16 wakati iliyotoka nje ikiwa tisa.

Kati ya washambuliaji wanne waliopo Yanga msimu huu ambapo jumla wamefunga mabao manne kati ya 14 yaliyofungwa na timu hiyo katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara, Mzize ndiye anayeongoza kwa mabao akiwazidi wenzake baada ya kufunga mawili akicheza mechi zote kumi kwa dakika 457.

Kwa upande wa Dube, amecheza mechi tisa kwa dakika 419, hajafunga zaidi ya kutoa asisti moja, huku Baleke katika mechi nne alizocheza kwa dakika 166, amefunga bao moja.

Kuelekea usajili wa dirisha dogo msimu huu, Yanga tayari ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na Bayo (26) ambaye ni mchezaji huru tangu alipoachana na MFK Vyskov inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Czech.

Bayo aliichezea MFK Vyskov mechi 42 na kuifungia mabao nane.

Kabla ya kujiunga na Vyskov, Bayo aliitumuikia Ashdod inayoshiriki Ligi Kuu ya Israel ambayo katika mechi 41 alizoichezea, alifunga idadi ya mabao nane katika mechi 41 huku akipiga pasi moja ya mwisho.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad