Mwanaume mmoja aitwaye Rohitash Kumar aliyetangazwa na Madaktari wa Hospitali ya Umma huko India kuwa amefariki dunia, ameamka katikati ya ibada ya mazishi muda mfupi kabla ya mwili wake kuchomwa moto.
Kumar mwenye umri wa miaka 25 ambaye amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kuzungumza na kusikia, alipata homa kali na kuwaishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Rajkiya Bhagwan Das Khetan katika Jimbo la Rajasthan Nchini India.
Afisa wa Hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa amesema Madaktari walitangaza kuwa Kumar alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitalini hapo akiwa na hali mbaya ambapo baada ya kauli ya Madaktari hao mwili wake ulipelekwa mochwari.
Mwili wa Kumar ulichukuliwa na Shirika la kijamii hadi eneo maalum la kuchoma maiti lakini kabla ya ibada ya kuchoma maiti kuisha, Mtu huyo alianza kupumua kwa kasi na kuzua taaruki miongoni mwa Watu waliohudhuria ibada hiyo.
“Akaanza kuusogeza mwili wake, tulishtuka na kuanza kukimbia” ameeleza Subhash Poonia ambaye alishuhudia tukio hilo na kusema kuwa waligundua kuwa Mtu huyo yupo hai na alirudishwa Hospitalini kwaajili ya matibabu.
Madaktari watatu wa Hospitali hiyo ambao walihusika katika mchakato wa kumpokea Kumar wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi ya mashtaka ya utovu wa nidhamu na kudharau majukumu yao ya kazi.