Mastaa Bongo Wamlilia Tessa wa Huba




MASTAA mbalimbali wa filamu, muziki na wadau wengine wa michezo wameonyesha kuguswa na kifo cha nyota mkongwe wa filamu nchini, Grace Mapunda ‘Mama Kawele’ au Tessa, jina alilokuwa akilitumia ndani ya tamthilia ya Huba, wakisema ameacha pengo kubwa katika fani ya sanaa kwa jumla.

Mama Kawele alikumbwa na mauti usiku wa kuamkia juzi Jumamosi alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mwananyamala baada ya kuugua na kulazwa hospitalini hapo kabla ya leo saa 10 jioni mwili wake kulazwa katika makaburi yal Kinondoni, huku wasanii wenzake na mastaa wengine wakimlilia.

Mkongwe huyo aliyeanza kufahamika kupitia tamthilia za kwenye runinga akiwa na kundi la Shirikisho Msanii Afrika lililokuwa likirusha michezo yake ITV kabla ya kugeukia filamu, mwili wake utaagwa na familia nyumbani kwake Sinza Vatican kabla ya kupelekwa Viwanja vya Leaders kuagwa na viongozi na wapenzi na mashabiki sambamba na wadau wengine kisha kupelekwa Kinondoni kuzikwa jioni.

Mara baada ya msiba huo, mastaa mbalimbali waliuelezea ni pigo kwa tasnia hiyo kwa namna enzi za uhai wake alivyojitoa na kushiriki kuigiza kama anafanya kweli na kusaidia wengine waliokuwa na ndoto za kufika mbali.

Wakali mbalimbali wa filamu, muziki na hata wanamichezo kama JB, Shamsa Ford, Hashim Kambi, Isarito walifika nyumbani kwa marehemu ulipo msiba huo na JB alisema;

“Alikuwa ni zaidi ya mama kama uigizaji na ufanisi wa kazi, mcheshi na aliyeipenda kazi yake, kuna kazi nyingine tumefanya naye kuanzia filamu hadi tamthilia kwa wanaozifuatilia wataelewa. Kwa kweli ni pigo kwetu, familia yake na wanafamilia nzima ya sanaa ya maigizo nchini.”

Mama Kawele alianza kuvuma miaka ya mwanzoni mwa 2000 akiwa na kundi la Shirikisho na kutamba na michezo kadhaa ikiwamo Tamu Chungu, Dumaza, Hatia, Gumbizi na mengine.

Enzi za uhai wake, alijaaliwa watoto wawili, Ritha na Happiness aliowahi kuigiza nao katika filamu ya Fake Smile. Watoto wake hao pia wanajihusisha na muziki wa kizazi kipya.

Mbali na kuigiza tamthilia, Mama Kawele alikimbiza sana katika filamu na baadhi ya kazi hizo ni House of Death, Hard Price, Nilindiwe, Kichupa, Majuto, Waraka Wangu, Mwaka wa Hasara, Chloroquine Love, Chungu ya Nafsi, Poor Minds, Jibu la Ndoto, Back to Life na nyinginezo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad