Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema usiku huu saa 12:54, Viongozi wa Chama hicho akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, wameachiwa bila masharti na Polisi Mkoani Songwe.
Mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA Jon Mrema amesema “Mdude hajaachiwa, RPC Kasema Wana mahojiano naye pamoja na Mtu mmoja ambaye aliumizwa vibaya na Polisi, tunaendelea kufuatilia hali ya afya ya Mdude”
Itakumbukwa Jeshi la Polisi Mkoani Songwe jana November 22,2024 lilitoa taarifa kuwa linawashikilia Wanachama wa CHADEMA ambao ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe, Joseph Mbilinyi (Sugu) Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Pascal Yohana Haonga, Mbunge Mstaafu CHADEMA Mbozi Mlowo, Mdude Mpaluka Nyagali, Apolinary Boniface Margwe, Afisa Habari CHADEMA na Adam Hassan Kasekwa, Mlinzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA.
Wengine waliokamatwa ni Paul Joseph Paul, Afisa wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Mbeya, Kelvin Keneth Ndabila, Afisa habari Kanda ya Nyasa, Mkazi wa Mbeya, Michael Laison Msongole, Mwenyekiti CHADEMA Wilaya ya Mbozi, Mlowo, Mohamed Abdilah Ling wanya, Mlinzi wa Mbowe Mkazi wa Dar es salaam, Alfan Hassan Mbire, Mlinzi wa Mbowe na Ezekia Elia Zambi, Mwenyekiti ACT Wazalendo Mkoa wa Songwe.
Polisi ilisema “Tukio hilo limetokea eneo la stendi ya zamani ya Mlowo Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe November 22,2024 majira ya 10:30 asubuhi baada ya CHADEMA kwenda kufanya mkutano wa kampeni eneo ambalo hawakupangiwa na ndipo Askari waliwapa amri ya kutawanyika lakini walikaidi ndipo Askari waliamua kuwatawanya kwa nguvu na ndipo walipoanza kurusha mawe na kuwajeruhi Askari wawili maeneo ya kichwani, usoni na puani na kwa sasa wanaendela na matibabu Hospitali ya Wilaya ya Mbozi”