Mo Salah Avunja Rekodi Tena Ligi Kuu England

 

Mo Salah Avunja Rekodi Tena Ligi Kuu England

Staa wa Liverpool, Mohamed Salah ameifikia rekodi ya Wayne Rooney ya Ligi Kuu England baada ya kufunga na kuasisti wikiendi iliyopita dhidi ya Aston Villa.


Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alitoa pasi kwa Darwin Nunez na akafunga bao mwenyewe katika ushindi wa Jumamosi dhidi ya Villa huko Anfield ambako aliifikia rekodi ya Rooney kwa kufunga na kutoa pasi ya bao akifanya hivyo katika mechi 35 tofauti za Ligi Kuu England.


Rooney ndio alikuwa kinara katika rekodi hiyo kabla ya Salah kuifikia na sasa staa huyo wa kimataifa wa Misri atahitaji kuivuka ili kuwa mchezaji pekee kuwahi kufanya hivyo katika historia ya EPL.


Bao na asisti ya Salah iliisaidia Liverpool kuendelea kujiwekea mizizi kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa ina pointi 28 baada ya kucheza mechi 11.


Salah yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na Liverpool na hadi sasa, hakuna ishara yoyote ya kusaini dili jipya.


Tangu Salah alipojiunga na Liverpool mwaka 2017 akitokea AS Roma kwa Pauni 43.9 milioni, Salah amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa kikosi cha majogoo wa Anfield akifunga mabao 221 na kutoa pasi za mabao 99 katika mechi 366 za michuano yote alizoicheza timu hiyo.


Salah atakuwa na nafasi ya kuvunja rekodi hii katika mchezo ujao dhidi ya Southampton utakaopigwa Novemba 24.


Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Villa, Liverpool ilipata pigo baada ya staa wao Trent Alexander anayecheza beki wa kulia kuumia na kutolewa uwanjani katika kipindi cha kwanza.


Hadi sasa haijajulikana majeraha aliyopata ni makubwa kiasi gani na atakaa nje kwa muda gani.


Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya staa huyo, kocha wa Liverpool Arne Slot alisema: "Ni ngumu sana kusema jeraha lake lina ukubwa gani kwa sasa, lakini inatia wasiwasi pale unapoona mchezaji anatoka katika kipindi cha kwanza, sikumtoa kwa sababu niliamua bali alitaka mwenyewe, alitoka kwa sababu alihisi kuna kitu hakipo sawa katika mwili wake jambo ambalo halitoi ishara nzuri, ni ngumu sana kusema zaidi ya hapa acha tusubiri na kuona baada ya vipimo. Nitashangaa sana nikimwona anacheza timu ya taifa wiki ijayo."


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad