Taifa Stars imeandika historia kwa kufuzu AFCON 2025 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Guinea. Kufuatia mafanikio haya, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. @samia_suluhu_hassan, ametangaza zawadi ya shilingi milioni 700 kwa timu hiyo kama pongezi kwa jitihada zao.
Rais Samia alisema: "Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini. Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa. Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo."
Rais pia ameonyesha msaada wake kwa sekta ya michezo kwa kuruhusu mashabiki kushuhudia mechi bila kiingilio, hatua ambayo iliwapa hamasa kubwa Stars. Ushindi huu ni hatua kubwa kwa soka la Tanzania kuelekea AFCON 2025 nchini Morocco.