Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amealikwa kushiriki mkutano wa viongozi wa G20 utakaofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil kuanzia Novemba 18 hadi 19, 2024 ukiwa na kaulimbiu inayosema 'Kujenga Ulimwengu wa Haki na Sayari Endelevu'.
Mwaliko huo umetolewa na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva ambapo Rais Samia atakuwa ni Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20 na Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa G20 tangu kupanuka kwa kundi hilo kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009.
Kulingana na taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa Novemba 13, 2024, ushiriki wa Rais Samia katika mkutano wa viongozi wa G20 unaashiria kuongezeka kwa ushawishi na mwonekano wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa na ukuaji wa diplomasia na sera za uwekezaji nje ya mipaka ya Tanzania.
“Ushiriki huu unaashiria kuongezeka kwa ushawishi na umaarufu wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa, ukizingatia juhudi za kidiplomasia za Rais Samia zinazolenga kuwawezesha vijana na wanawake pamoja na kushughulikia changamoto za kitaifa na kikanda kama vile mpito wa nishati, umasikini, njaa, ukosefu wa ajira kwa vijana, athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, na usalama wa chakula ambazo pia ni kipaumbele katika Mkutano wa Viongozi wa G20 wa mwaka 2024”, imeeleza taarifa hiyo.
G20 inajumuisha nchi 19 ambazo ni Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Jamhuri ya Korea, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani pamoja na mashirika mawili ya kikanda ambayo ni Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU) hadi mwaka 2023
Sifa mojawapo ya nchi wanachama wa G20 ni kwamba zinawakilisha takribani asilimia 85 ya Pato la kimataifa, zaidi ya asilimia 75 ya biashara za kimataifa na karibu theluthi mbili ya watu duniani, na kwa hatua hii ya Rais Samia kualikwa imeelezwa kuwa fursa kubwa ya kufungua milango ya uwekezaji kwa Tanzania.