Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema wakati anaoneshwa ghorofa lililoporomoka Kariakoo leo November 20,2024 amebaini kwa jinsi lilivyojengwa hapakuwa na usimamizi mzuri wakati wa ujenzi wake na kwamba kuna viashiria vya kuwepo kwa mapungufu ya kiutendaji kuanzia kwa Wamiliki wa jengo hadi kwa Mamlaka za Serikali zilizowapa vibali vya ujenzi.
Akiongea leo akiwa Kariakoo, Rais Samia amesema “Tukio hili limetupa ujumbe mkubwa wa kuangalia usalama wa majengo yetu Kariakoo, wakati naoneshwa lile jengo ukiliangalia lilivyojengwa, kuta zake na nondo pale hapakuwa na usimamizi mzuri, jengo halikusimamiwa vizuri, limejengwa jengo kubwa bila kuona madhara yatakayotokea baadaye”
“Tukio hili ukiangalia kwa macho tu lina viashiria vya kuwepo kwa mapungufu ya kiutendaji hivyo nitoe wito kila Mtu atimize wajibu wake ipasavyo, ukiangalia jengo lile lilipewa vibali kutoka Serikalini vya ujenzi lakini jengo lile halikutazamwa ubora wake wakati wa ujenzi, niwaombe wote tunaohusika Serikali Kuu, Halmashauri na Wananchi wote kwa ujumla tuseme kwa pamoja kwamba matukio ya aina hii yasijirudie”