Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasihi Wananchi kujiepusha na vitendo vya uchochezi, vurugu au uvunjifu wa sheria kesho November 27,2024 wakati wa kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akihutubia Taifa leo kutokea Ikulu Chamwino Dodoma , Rais Samia amesema “Ndugu Wananchi kesho Jumatano November 27,2024 ni siku ambayo tutaendeleza utamaduni wetu wa kupata Viongozi wetu kwa njia ya Uchaguzi, tutawachagua Viongozi wetu wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hii ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania mwenye fursa ya kupiga kura kuchangia maendeleo ya Nchi kwa njia ya kidemokrasia kwa kuchagua Kiongozi mwenye sifa”
“Hii ni fursa ya kuhakikisha kuwa maamuzi yanayohusu Jamii zetu yanatokana na mahitaji halisi ya Wananchi, kila kura itakayopigwa ina maana na itasaidia kufanikisha azma yetu ya kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo kwa wote, Uchaguzi ni haki yetu na ni jukumu letu kuhakikisha tunatumia haki hiyo kwa amani na utulivu, hivyo niwasihi Wananchi tujiepushe na vitendo vya uchochezi, vurugu au uvunjifu wa sheria, amani ni urithi wetu wa thamani na ni wajibu wetu kuilinda kwa gharama yoyote ile”
“Aidha ni muhimu kuheshimu maamuzi ya Wapiga kura, kwani demokrasia yenye nguvu hujengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano, niwakumbushe Wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura, kuhakikisha wanajitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba, niwasihi chagueni Viongozi waadilifu, wabunifu na wenye maono ya kuendeleza jamii zetu, kumbukeni kila kura ina umuhimu mkubwa katika kuamua mustakabali na maendeleo yetu na Taifa kiujumla”
“Kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea na Wasimamizi wa Uchaguzi niwakumbushe kuzingatia sheria na kanuni za Uchaguzi, na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na Wadau”