Siri ya Wakurya kuwa wababe, wakali na wajasiri

Siri ya Wakurya kuwa wababe, wakali na wajasiri


Hata hivyo, Wakurya wengi wanapatikana katika wilaya za Tarime, Serengeti na sehemu za wilaya za Rorya na Butiama lakini pia wanaishi katika wilaya zingine za mkoa huo.


Mbali na kupatikana mkoni humo pia kabila hili lenye koo zaidi ya 10, ni moja ya makabila makubwa ndani ya mkoa huo na pengine nchini pia.


Ukubwa wa kabila hili mara nyingi umekuwa ukiwachnaganya watu wengi hasa wasiokuwa wenyeji ama wakazi wa mkoa wa Mara, hadi kudhani watu wa Mara wote ni Wakurya, jambo ambalo sio kweli kwani mkoa huu una utajiri wa makabila mengi yakiwamo makubwa kwa madogo.


Hawa ndio Wakurya


Kama ilivyo kwa makabila mengine nchini, kabila la Wakurya pia lina sifa zake zinazolifanya kuwa tofauti ama kufanana na makabila mengine.


Kabila hili linadaiwa kuwa na watu wakali, wajasiri na katili ingawa wenyewe wanasema wao sio katili bali ni watu wenye upendo. Hata hivyo, wanakiri kuwa wao ni wakali na walio na ujasiri wa hali ya juu


Mzee Timothy Itembe anasema zipo sababu nyingi zinazochangia Wakurya kuwa wakali na wajasiri, lakini kubwa ni imani, mazingira na vyakula.


Anasema kihistoria Wakurya, chimbiko lao ni Sudan hivyo katika harakati za kuhama ama kutafuta maeneo na makazi mengine, walisafiri kutoka nchini humo na kuingia nchini huku wengine wakiendelea hadi nchini Kenya.


"Wakiwa njiani popote walipokuwa wanapiga kambi hawakuruhusu jamii yoyote kukaa pale, hivyo walipigana nao na kuwafukuza wakiamini wao ndio wenye haki na eneo hilo na hakuna kabila lolote lililotakiwa kuishi hapo, na hii iliwajengea ujasiri mkubwa,"anasema.


Anasema mbali na safari, pia suala la tohara ya asili ni moja ya kichocheo cha ujasiri na kujiamini kwa watu wa kabila hilo.


Anasema tohara ya asili inafanywa kwa kukatwa ngozi ya uume kwa kutumia kisu maalum bila kutumia ganzi huku anayetahiriwa akitakiwa kuonyesha ujasiri wa hali ya juu.


"Kile kitendo cha kukatwa bila ganzi na wewe hautikisiki wala kukunja uso ni moja ya kichocheo kikubwa cha ujasiri na ukali, kwani ukitoka hapo unakuwa na ujasiri wa hali ya juu," anaeleza Mzee Itembe.


Anaongeza: ‘’Sio kwamba wakati wa tohara hakuna mamumivu la hasha! Maumivu yapo tena ni makali mno lakini kijana anajengwa kisaikolojia kukabiliana na hali hiyo na kwamba endapo ataonyesja dalili za kusikia maumivu kwa namna yoyote ile, basi hali hiyo itasababisha dharau na dhihaka kwake na kwa familia yake pia.’’


Anasema kutokana na hali hiyo kijana anajitahidi ili yeye mwenyewe asidharauliwe au kudhihakiwa na wala familia yake pia isidharaliwe na kudhihakiwa, hivyo ni lazima aonyeshe kuwa yeye ni jasiri kwa kukaa kimya wakati wa kutahiriwa bila kutikisika wala kukunja uso achilia mbali kulia kabisa kama ishara ya kuhisi maumivu.


Anasema baada ya kupitia tohara, Wakurya wengi wamekuwa wakijiona majasiri wa hali ya juu, huku wakiamini kuwa hakuna kabila linaloweza kulingana nao hususan makabila ambayo tohara hufanyika kwa njia za kisasa, ikiwa ni pamoja na kuchomwa sindano ya ganzi kabla ya kutahiriwa.


Anasema zamani pia wazee wa Kikurya walikuwa na utaratibu wa kuwanywesha watoto wao aina fulani za mitishamba, ambayo walikuwa wakiamini kuwa inachochea ujasiri na ukali baada ya kutumiwa.


"Kuna aina mbalimbali ya miti, nakumbuka mmoja unaitwa 'ekerore' kwa Kikurya sijui kwa Kiswahili unaitwaji huu mti, ni mchungu sana ukiunywa yaani hadi sauti inabadilika," anasema.


Anasema ingawa kwa sasa utamaduni huo wa kunyweshwa miti michungu na mikali ni kama unapotea, kwa kiasi kikubwa ulikuwa unachochea na kuwajengea tabia ya ukali na ujasiri vijana wa Kikurya hali ambayo walikuwa wanakuwa nayo hadi wanapozeeka.


Anasema miti hiyo mbali na kutumika kama kichocheo cha ujasiri na ukali, pia ilikuwa inatumika kama tiba ya asili kwa magonjwa mbalimbali.


Mzee Itembe anasema vipo vyakula vichungu ambavyo pia vinatumiwa na watu wa kabila hilo na kwa namna moja ama nyingine, vinachochea ujasiri na ukali kwa watu wa kabila hilo.


Anataja aina ya vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kichuri ambacho hutumiwa sana hasa kwenye mapishi na ulaji wa kitoweo aina ya nyama. Kichuri hutumika kama kiungo kuboresha ladha ya nyama kavu au ya kupika.


Kichuri hupatikana kwenye utumbo wa mbuzi au ng'ombe, ni kinyesi laini ambacho kinakuwa hakijawa tayari kutolewa nje na mnyama husika kama kinyesi, baada ya kutolewa kwenye utumbo kinachujwa na kuchanganywa na nyongo na kuchemshwa kisha kutumika ambapo mtumiaji anaweza kuongeza viungo kama pilipili na limao na hutumika kwenye nyama ya kuchoma au unaweza kupika na nyama moja kwa moja baada ya kukiandaa.


"Kuna kitu pia tunakiita hirizi ya simba hiki ni kitu huwa kinatapikwa na simba akitaka kufa na huwa anakitapika kwa kujificha, sasa Mkurya akikipata anakuwa nacho mwilini au anakimeza na tunaamini kinasaidia sana kufanya mtu kuwa mkali na jasiri sana," anaeleza.


Ulaji nyama nyekundu


Mzee mwingine Hunga Marwa, anasema Wakurya sio katili bali ni wakali na wajasiri na kwamba sababu nyingine inayochangia hali hiyo ni ulaji wa nyama nyekundu.


Anasema kwa Wakurya nyama nyekundu ni moja ya kitoweo kinachopendwa sana na kwamba katika maisha ya kawaida ya Mkurya hasa kama familia ina uwezo wa kitoweo hicho, kinaweza kutumika zaidi ya mara tano kwa wiki.


Marwa anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya ulaji wa nyama na hasira, ukali na ujasiri huku akisema kuwa hata kwenye majeshi suala la ulaji wa nyama nyekundu huwa linasisitizwa na kupewa kipaumbele.


Anatolea mfano wa wanyama wanaokula nyama kama simba, chui, mbwa na wengine wengi ambao kwa asili yao ni wakali, ni wanyamaa wanaokula nyama.


"Wewe si unaona simba alivyo mkali au chui hii. Hii yote ni kwa sababu wanakula nyama tofauti na wanyama kama swala, pundamilia na wengineo wanaokula mimea," anasema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad